Mastaa Yanga wapewa masharti

Muktasari:

  • Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo ni kwamba matajiri wao wamemaliza kesi ya madai ya fedha zoteĀ  za bonasi za mechi mbili za kimataifa moja wakicheza ugenini na nyingine wakishinda nyumbani dhidi ya Real Bamako ya Mali

YANGA ipo kambini ikianza safari ya kuusaka ushindi muhimu dhidi ya wageni wao US Monastir lakini kwenye akaunti zao kumejaa manoti ya bonasi za mechi zao walizoshinda huku mabosi wao wakiweka wazi mazito ya wachezaji wao ambayo yatawachongea Waarabu hao huku pia wakieleza maisha matamu ndani ya kikosi hicho.

Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo ni kwamba matajiri wao wamemaliza kesi ya madai ya fedha zoteĀ  za bonasi za mechi mbili za kimataifa moja wakicheza ugenini na nyingine wakishinda nyumbani dhidi ya Real Bamako ya Mali.

Mzuka huo ukaambatana na maamuzi mazito ambayo yatawafanya wachezaji hao kuusaka ushindi mbele ya Monastir wakiambiwa kuwa hawatapokea chochote nje ya ushindi kwenye mchezo wa Jumapili Machi 19.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo ameliambia Mwanaspoti kuwa hakuna ambacho wanakizungumza sasa na wachezaji wao nje ya kutaka ushindi mbele ya Monastir wanaoongoza kundi lao kwenye mechi za Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Gumbo amefichua kwamba kuanzia mchezo uliopita dhidi ya Real Bamako ya Mali wachezaji wao walifutiwa bonasi ya matokeo ya sare ya nyumbani lengo likiwa kutaka ushindi pekee nyumbani kwa sasa.
Awali Yanga kupitia rais wao Hersi Said alitangaza kuwa kikosi chao kitakuwa na bonasi mpya za matokeo ya sare katika mechi za hatua ya makundi.

"Tunaendelea na maandalizi kama kamati ya mashindano, hakuna ambacho tunafikiria sasa nje ya ushindi wa mechi hii dhidi ya Monastir, hii ni mechi yetu kama fainali na hilo wachezaji wetu wanalielewa,"alisema Gumbo ambaye amekuwa akiiongoza kamati hiyo kwa mafanikio.

"Hii ni mechi ambayo nayo tunahitaji ushindi na sio matokeo mengine, kwenye mchezo wetu uliopita tuliwatangazia wachezaji wetu kwamba mchezo wao wa mwisho kupata bonasi kwenye matokeo ya sare ni ile mechi tuliyocheza Mali baada ya hapo hatutakuwa na bonasi kwenye sare hasa hizi mechi za nyumbani.

"Hii mechi watapata bonasi kwa ushindi pekee kama ambavyo tulifanya katika mchezo uliopita wa nyumbani, washinde waendelee kuogelea fedha zao hakuna wanachotudai.

Ingawa Gumbo hakutaka kuweka wazi lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa wachezaji hao wamevuna kiasi kisichopungua sh 150 milioni kwa kushinda mechi moja ya nyumbani na kupata sare ugenini, fedha ambazo tayari walishalipwa tangu mwanzoni mwa wiki hii.

Aidha Gumbo aliongeza kuwa katika kuhamasisha ushindi kutoka kwa wanachama wao kamati yao itakuwa na kikao kesho Alhamisi Machi 16 na uongozi wa matawi yao kuhakikisha wanaunganisha nguvu na wanachama wao.