Mauritania yapata ushindi wa kwanza CHAN, Afrika ya Kati yakaribia kuaga
Muktasari:
Mauritania imebakiza mchezo mmoja kwenye mashindano ya CHAN ambao itacheza na Burkina Faso.
Mauritania imeonja ushindi wa kwanza katika Fainali za CHAN 2024 baada ya leo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kabla ya mechi ya leo, Mauritania ilivuna pointi moja tu katika mechi mbili za kwanza ilizocheza dhidi ya Madagascar na Tanzania ‘Taifa Stars’.
Mchezo dhidi ya Madagascar ilitoka sare tasa na kisha ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Taifa Stars.
Bao hilo la mapema la dakika ya tisa kupitia kwa Ahmed lilitosha kuipa ushindi huo Mauritania leo.
Japokuwa Afrika ya Kati ilimiliki mpira zaidi kwa asilimia 57 dhidi ya asilimia 43 za Mauritania haikufua dafu mbele ya ngome imara ya Mauritania.
Afrika ya Kati ilipiga mashuti 16, lakini ni matatu ndiyo yaliyolenga lango, ilikosa makali katika umaliziaji.
Mauritania katika mechi hiyo ilipiga mashuti saba na la kwanza lililenga lango ndilo lililozaa bao.
Ufanisi wa hali ya juu hapana shaka Kocha wa Mauritania atakuwa na furaha jinsi vijana wake walivyotimiza majukumu yao.
Timu hiyo ilijilinda vyema na ilipanga vizuri mashambulizi yake muda mwingi wa mchezo.