Mbangula afande aliyemfunga Manula mabao matatu

Muktasari:

  • Siku moja kabla ya mchezo huo, Ahmed kama kawaida yake, alitoa tambo kwamba kwa uimara wa ngome ya Simba ni ngumu kwa Mbangula kupenya mbele yao, maneno yaliyogeuka utani baada ya mchezaji huyo kuwafunga.

Kazi nzuri haiwezi kumtupa mtu, ndicho kilichotokea kwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula aliyegeuka habari ya mjini, baada ya kuifunga Simba.

Machi 6, Simba ilidondosha pointi tatu mbele ya Prisons (Uwanja wa Jamhuri), ikiwafunga  mabao 2-1, mfungaji akiwa ni  Mbangula na sababu ya kuzungumziwa mitandaoni ni maneno ya Ahmed Ally,Mkuu wa Idala ya Habari na mawasiliano wa Simba.

Siku moja kabla ya mchezo huo, Ahmed kama kawaida yake, alitoa tambo kwamba kwa uimara wa ngome ya Simba ni ngumu kwa Mbangula kupenya mbele yao,maneno yaliyogeuka utani baada ya mchezaji huyo kuwafunga.

Spoti Mikiki limefanya mahojiano na Mbangula ambaye ni mara ya pili kuifunga Simba ya kwanza ilikuwa Januari 22/2022, Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga  mchezo ulimalizika kwa bao 1-0 na ya pili ni hiyo ya juzi ya mabao 2-1.

Kipa wa Simba, Aishi Manula ni kama ana bahati mbaya na Mbangula kwani mechi zote mbili alikuwa golini na hivyo ameshatunguliwa mabao matatu na straika huyo.

Anaulizwa unayazungumziaje maneno ya Ahmed dhidi yako? Anajibu:"Ni mshikaji wangu, kabla ya mechi nilimtumia ujumbe wa maandishi nilioandika hivi 'Kaka wa magari' akajibu tuonane Jamhuri akaweka na nukta ili nisiendelee kumsemesha.

Anaongeza "Baada ya hapo nikaachana naye, kwani namfahamu utani wake tangu yupo Azam FC,niliiona video yake baada ya mechi, nikacheka sana, siwezi kusema nayachukulia vibaya, yupo kazini kuisemea timu yake, kama ambavyo msemaji wetu anavyotusemea sisi.

"Mpira ni mchezo wa makosa, mabeki wa Simba wakayafanya tukayatumia kuwaadhibu, ila naheshimu viwango vya kina Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Shomari Kapombe, ndio maana wanaitumikia timu yetu ya taifa kwa sababu ya uwezo wao."

Kitu kingine wasichofahamu wengi, Ahmed anakubari sana uwezo wangu, wakati mwingine maneno yake yananipa nguvu ya kupambana.


Msimu huu 
Mbangula mwenye mabao saba Ligi Kuu Bara, anauzungumzia msimu huu ni mgumu, ila uwepo wa kocha wao mpya, Hamad Ally anaona umebadili upepo, wanajisikia morali ya kupambana.

"Kocha Ally katujenga kiakili, kwa sasa morali zetu zipo juu, hamasa imerejea, tunatarajia msimu huu hatutamaliza kinyonge, tofauti na msimu  uliopita ambao tulicheza mtoano dhidi ya Mtibwa Sugar ikatushinda mabao 3-1 nyumbani na ugenini, kisha tukamaliza na JKT Tanzania,"anasema.


Soka limempa ajira

 "Nimeajiriwa na Magereza nikitokea JKT kambi ya 82KJ Bulombora, mpira nimecheza nikiwa muajiriwa, hivyo siwezi kusema kuna mtu amenivutia kuupenda moja kwa moja,"anasema.

Anaulizwa je unaweza ukakacha jeshi endapo Simba na Yanga zikileta ofa nono? Anajibu "Siwezi kuacha kazi yangu ya jeshi, kitu ninachokitamani kwa sasa nikuichezea Stars."

Anaongeza "Nimeanza kucheza mpira ndani ya ajira, niliamini ninaweza nikaonyesha kipaji na nakionyesha,nalitumikia taifa langu kupitia kazi hii."

Lakini kwa upande wa washambuliaji anaowakubali anamtaja John Bocco wa Simba namna alivyoonyesha muendelezo wa kiwango chake, anaona anastahili kupewa heshima yake.

Ukiachana na hilo, kitu ambacho hatakaa akisahau kwenye maisha yake ni majeraha ya kichwa aliyoyapata mazoezini baada ya kugongana na kipa Hassan Msham, wakati tunajiandaa kucheza dhidi ya KMC.

"Nilipelekwa hospitali baada ya tukio hilo, niliambiwa fuvu limebonyea ndio maana nilikuwa navaa helmet,"