Mbeya City, Prisons zatua Kanda ya Ziwa kuvuna pointi

Muktasari:

Mechi ya kwanza kwa timu hizo zitacheza mkoani Shinyanga ambapo, Mbeya City itakuwa na kibarua cha kuikabili Stand United   siku ya Jumamosi huku Mwadui FC ikiikaribisha Prisons, Jumapili kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Klabu za Tanzania Prisons na Mbeya City za jijini hapa, zimeondoka kwa pamoja  kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya mechi zao  huku zikiwa na matumaini kibao ya kufanya vizuri wakiwa ugenini.

Mechi ya kwanza kwa timu hizo zitacheza mkoani Shinyanga ambapo, Mbeya City itakuwa na kibarua cha kuikabili Stand United   siku ya Jumamosi huku Mwadui FC ikiikaribisha Prisons, Jumapili kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Prisons imeondoka na kikosi cha wachezaji 24 pamoja na viongozi sita ambapo City wenyewe walitarajia kuondoka jana jioni na msafara wa timu ya watu 31 wakiwemo viongozi.

Kocha Msaidizi wa City, Mohammed Kijuso alisema ingawa mpira ni dakika 90 lakini wamejipanga kucheza soka safi na kuongeza pointi na kujiweka katika nafasi nzuri kimsimamo.

Naye Kocha Mkuu wa Prisons, Abdallah Mohammed alisema pamoja na ligi ya msimu huu kuonyesha ugumu wake lakini waliojipanga vyema ndiyo wanaong'ara.