Mbeya City yalamba mkataba mnono

Muktasari:

KLABU ya Mbeya City imepata udhamini kutoka kampuni ya kubashiri michezo mitandaoni ya Parimatch ambao unalenga maeneo matatu tofauti.

KLABU ya Mbeya City imepata udhamini kutoka kampuni ya kubashiri michezo mitandaoni ya Parimatch ambao unalenga maeneo matatu tofauti.

Parimatch imetoa udhamini kwa Mbeya City kuwapa fedha ambazo hawakuweka hadharani kiasi kamili, pia kampuni hiyo itawapatia vifaa vya michezo na kukarabati uwanja wa Sokoine eneo la kukaa benchi la ufundi.

Udhamini huo wa Parimatch na Mbeya City unakuwa wa awamu ya pili baada ya kufanya hivyo mara ya kwanza misimu mitatu iliyopita.

Ofisa habari wa Parimatch, Ismail Mohamed anasema thamani ya mkataba huo pande zote mbili zimekubaliana na unalenga maeneo matatu tofauti.

"Thamani ya mkataba huu ni siri baina ya kampuni na Mbeya City lakini niweke wazi utalenga zaidi kutoa vifaa vyote vya mpira, kugharamia safari za timu wanapokwenda kucheza mechi za ugenini, kukarabati eneo la kukaa mabenchi ya ufundi kwenye Uwanja wa Sokoine ambao unatumiwa na Mbeya City," anasema Mohamed.

“Mbali ya kuwapa udhamini huo wa mwaka mmoja Mbeya City, Parimatch wapo kwenye mazungumzo na klabu nne za ligi daraja la kwanza kuangalia uwezekano wa kuwadhamini.”

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe anasema udhamini utawasaidia sana katika kufikia lengo lao la kufanya vizuri msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara na ASFC.

“Tunaamini katika udhamini huu utakwenda kutupa faidi katika kujenga na kutengeneza kikosi muda wote ndani na nje ili kufikia malengo ya kurudisha makali ya kikosi cha Mbeya City,” anasema Kimbe na kuongeza;

"Msimu uliopita ulikuwa mgumu tulicheza bila kuwa na mdhamini, ujio wa Parimatch umekuja wakati mzuri, tunafahamu ligi msimu huu itakuwa ngumu zaidi, uwepo wa Parimatch utatusaidia kufikia malengo yetu msimu huu, tunataka kumaliza ligi kwenye nafasi za juu,"

“Udhamini huu ni ushirikiano mzuri baada ya kuwadhamini miaka miwili iliyopita, ilifanya sisi kutosita kuwakubali Parimatch mbele ya makampuni mengine, tunawafahamu weledi wao wa kusimamia mikataba ya udhamini," anasema Kimbe.

Kuhusiana na maandalizi ya msimu mpya, Kimbe anasema klabu hiyo ipo kambini huku ikiwa na maingizo mapya ya wachezaji.

"Hatukuwa na msimu mzuri msimu uliopita, timu ilimaliza sehemu mbaya, msimu huu tumejipanga kuhakikisha hatufanyi vibaya tena," anasema Kimbe.