Mbinu kuzibeba Simba, Mtibwa

Dar es Salaam.Wakati Simba na Mtibwa zikicheza fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa mara ya tatu, baada ya ile ya mwaka 2008 na 2015, rekodi zinaibeba Simba katika mchezo huo.

Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Amaan unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu hizo zenye historia ya kucheza fainali ya Kombe la Mapinduzi mara nyingi zaidi, Simba ikicheza mara sita na Mtibwa mara tano.

Simba ilitinga fainali kwa kuiondosha Azam wakati Mtibwa ikiifunga Yanga katika mechi za nusu fainali.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck na Zuberi Katwila anayeinoa Mtibwa kila mmoja amejinasibu kuondoka na taji hilo msimu huu licha ya rekodi kuibeba Simba.

Katika mechi 10 za mwisho ambazo timu hizo zimekutana, Simba imeshinda saba, sare mara tatu na katika michezo 20 Simba imeshinda mechi 14, sare tatu na kufungwa tatu.

Katika mechi ya Kombe la Mapinduzi timu hizo zilikutana mara ya kwanza kwenye fainali mwaka 2008 na Simba ilitwaa ubingwa kwa ushindi wa bao 1-0 na mwaka 2015 iliichapa Mtibwa kwa penalti 4-3 baada ya kutoka suluhu.

Pia katika mechi 10 za ligi baina ya timu hizo, Simba imefunga mabao 12 Mtibwa imepachika mawili kupitia kwa Riphat Msuya na Stamili Mbonde.

Katika mechi hizo Emmanuel Okwi alifunga mabao manne na mengine yalifungwa na Meddie Kagere, Miraji Athumani, John Bocco, Clatous Chama, Hamis Kiiza, Luadit Mavugo, Ibrahim Ajibu na Mohammed Banka.

Leo itakuwa ni fainali ya 14 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2007 ambapo Yanga ilitwaa ubingwa kwa kuichapa Mtibwa mabao 2-1.

Mtibwa iliyotangulia kuingia hatua hiyo ilikata tiketi kwa kuilaza Yanga kwa penalti 4-2 baada ya timu zote kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1.

Kikosi cha Katwila juzi kilifanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Mau Tse Tung lakini jana kilipumzika kusubiri mchezo huo.

Mtibwa inatambua ubora wa Simba na jinsi walivyo na kikosi imara, lakini Katwila amefunguka kuwa wako tayari kwa mchezo huo.

Katwila ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo, alisema Simba inaongoza Ligi Kuu, kufika fainali na ubora wa wachezaji wao kutafanya mchezo huo kuwa na ugumu lakini wamejipanga kutoa upinzani ili kupata matokeo mazuri.

Alisema ameiona timu hiyo ikiumana na Azam na anajua mbinu za wapi wanapata nguvu ya kuwa bora na tayari wamejipanga kuwadhibiti.

“Tunakutana na Simba lakini sote tunajua ubora wa Simba ambayo licha ya kufika fainali hapa pia kule nyumbani wanaongoza ligi sio timu ya kubeza.

“Hii ni mechi ya fainali ambayo lazima mshindi apatikane, kikosi changu kipo tayari kwa vita hii ya uwanjani na vijana wangu tumewapa mbinu ya kuweza kuwadhibiti wapinzani wetu na kufanikiwa kushinda,”alisema Katwila.

Simba baada ya kucheza kwa kiwango bora katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Azam, imetamka hawawezi kufanya makosa kama waliyofanya kwa watani wao wa jadi Yanga.

Januari 4 Simba ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Yanga licha ya kutangulia kuongoza kwa mabao 2-0.

Kauli ya Simba imetolewa na kocha msaidizi Selemani Matola ambaye alisema hawana nafasi ya kuidharau Mtibwa kwa kuwa ni timu bora yenye uzoefu na mashindano makubwa.

Matola alisema watapanga kikosi imara ambacho kitakuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa huo ambao utakuwa wa kwanza mwaka huu.

Baada ya kuitupa nje Azam kwa mikwaju 3-2, Matola alisema wataingia katika mchezo huo wakiwa na mbinu zote katika kusaka ushindi ndani ya dakika 90.

Nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo alisema wamejiandaa kwa penalti endapo mchezo huo utaamuliwa kwa njia hiyo baada ya dakika za kawaida kumalizika.

“Mtibwa si timu ya kuidharau kama mnavyoona waiwatoa Yanga na hii ni fainali kwa hiyo kila timu ina nafasi muhimu ni maandalizi.

“Simba tuko tayari kwa mchezo wa fainali tumekiandaa kikosi vyema kucheza fainali, tunataka kuchukua taji hili kuendelea kuweka rekodi yetu bora katika mashindano haya,”alisema kocha huyo wa zamani wa Polisi Tanzania.