Ibenge aachana na Al Hilal, njiani Azam FC

Muktasari:
- Ibenge ameiwezesha Al Hilal kushinda taji la Ligi Kuu Sudan, Kombe la Ligi (Sudan Super League) na ubingwa wa heshima wa Ligi Kuu Mauritania iliyoshiriki 2024-2025 kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyopo kwao Sudan.
Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Al Hilal Omdurman ya Sudan, Florent Ibenge amewashukuru wafanyakazi, wachezaji, watendaji, mashabiki na watu wote wa Sudan kwa kipindi cha miaka mitatu aliyofanya nao kazi, huku akiwaambia atabaki katika mioyo yao.
Hatua ya kocha huyo kuaga inajiri baada ya jana Mtendaji Mkuu wa Al Hilal, Hassan Ali Issa kueleza wamefikia uamuzi wa kuchana naye kutokana na mkataba wake kuisha, huku akiwa tayari kwa ajili ya kupata changamoto sehemu mpya.
Uamuzi wa Ibenge unakuja baada ya kocha huyo mwenye mafanikio makubwa Afrika kufikia makubaliano ya kuifundisha Azam FC msimu ujao, akichukua nafasi inayoachwa na Rachid Taoussi ambaye ni raia wa Morocco.
Katika kipindi cha misimu mitatu aliyoitumikia Al Hilal, Ibenge ameiongoza kwenye mechi 91 ambapo kati ya hizo ilishinda 55, sare 20 na kupoteza 16, huku kikosi hicho kikifunga mabao 158 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 62.
Ibenge ameiwezesha Al Hilal kushinda taji la Ligi Kuu Sudan, Kombe la Ligi (Sudan Super League) na ubingwa wa heshima wa Ligi Kuu Mauritania iliyoshiriki 2024-2025 kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyopo kwao Sudan.
Kwa upande wake Taoussi aliyezifundisha timu mbalimbali zikiwemo RS Berkane, FAR Rabat, Raja Casablanca, ES Setif, Olympique Club de Khouribga na Wydad Casablanca alitambulishwa Azam FC Septemba 7, 2024, akichukua nafasi ya Msenegali Youssouph Dabo.
Dabo alijiunga na Azam Mei 1, 2023 baada ya kuachana na ASC Jaraaf de Dakar ya kwao Senegal akisaini kandarasi ya miaka mitatu kuifundisha akichukua nafasi iliyoachwa na Kally Ongala.
Taoussi ameiwezesha Azam kumaliza nafasi ya tatu na pointi 63 katika Ligi Kuu msimu uliomalizika baada ya kushinda mechi 19, sare sita na kupoteza tano, huku ikikata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.