Mcheza judo ajiondoa Olimpiki kumkwepa mpinzani kutoka Israel

Muktasari:

Mcheza judi wa Algeria, Fethi Nourine amejiondoa katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo kabla ya kuanza kushiriki baada ya ratiba kuonyesha uwezekano wa kukutana na mpinzani kutoka Israel.

Tokyo, Japan (AFP)
Mcheza judi wa Algeria, Fethi Nourine amejiondoa katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo kabla ya kuanza kushiriki baada ya ratiba kuonyesha uwezekano wa kukutana na mpinzani kutoka Israel.
Nourine alitazamiwa kukutana na mpinzani kutoka Sudan, Mohamed Abdalrasool Jumatatu katika mchezo wa raundi ya kwanza, na angekutana na Musraeli Tohar Butbul katika raundi inayofuata.
Akizungumza katika televisheni ya serikali ya Algeria jana Alhamisi jioni, Nourine alisema msimamo wake wa kisiasa wa kuunga mkono Palestina, unafanya kusiwe na uwezekano kwake kushindana na Muisraeli.
"Tulifanya kazi kubwa kufuzu Olimpiki... lakini maslahi ya Palestina ni makubwa kuliko yote hayo," alisema akiongeza kuwa uamuzi wake "ni wa mwisho".
Hii si mara ya kwanza kwa Nourine kujiondoa mashindanoni kuepuka kukutana na mpinzani kutoka Israel, baada ya kujiondoa katika michuano ya ubingwa wa dunia iliyofanyika mwaka 2019 jijini Tokyo.
Wacheza judi wa Iran pia wako katika mazingira magumu kwa kukataa kupambana na wapinzani kutoka Israeli.