Mechi Simba na Yanga kurudiwa, viingilio kutorudishwa

Mechi Simba na Yanga kurudiwa, viingilio kutorudishwa

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amehitimisha sakata la kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga na kuafikiana na pande zote mbili kuwa mechi hiyo itarudiwa.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amehitimisha sakata la kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga na kuafikiana na pande zote mbili kuwa mechi hiyo itarudiwa.

Pia, amewaomba viongozi wa klabu na mashabiki kuwa watulivu na kuiamini Serikali kuwa ilikuwa na nia njema na sababu za msingi iliposhauri mechi isogezwe mbele kabla ya kujitokeza mazingira

yaliyosababisha Bodi ya Ligi kulazimika kuuahirisha mchezo.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyokuwa ichezwe Mei 8,  2021  kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam iliahirishwa na itatangazwa tarehe mpya baada ya kikao kilichofanyika jana usiku Jumatatu Mei 10, 2021.

Katika kikao hicho, kilichohudhuriwa na vigogo wa klabu hizo kongwe na wale wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na bodi ya Ligi, wizara imetoa maagizo manne leo Jumanne Mei 11, 2021

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano serikalini, John Mapelele  leo imesema kufuatia maelekezo yaliyotolewa bungeni jana na waziri mkuu, Kassim Majaliwa, usiku huohuo waziri Bashungwa alifanya kikao cha mashauriano na pande zote zinazohusika.

Kikao hicho kilichowashirikisha viongozi kutoka BMT na wizarani, TFF iliwakilishwa na rais wake, Wallace Karia na Katibu mkuu, Wilfred Kidau; mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Stephen Mguto na mtendaji wake, Almas Kasongo.

Simba iliwakilishwa na mwenyekiti, wa Klabu, Murtaza Mangungu na mtendaji mkuu, Barbara Gonzalez na mjumbe wa bodi ya klabu, Zacharia Hanspoppe huku Yanga ikiwakilishwa na mwenyekiti wake,  Dk Mshindo Msolla; mjumbe wa kamati tendaji, Bahati Mwaseba na kaimu

katibu mkuu, Haji Mfikirwa.

Taarifa ya wizara ilisema makubaliano yamefikiwa mechi hiyo irudiwe, TFF na bodi wakae haraka iwezekanavyo na kutoa tarehe ya kurudiwa mechi hiyo.

"Mashabiki waliokata tiketi waziri ameagiza kituo cha kitaifa cha data wanaosimamia mfumo wa N-Card kuwarejeshea tiketi zao kwenye mfumo wa kadi za kuingilia uwanjani mashabiki wote 43, 947, ili tiketi hizohizo za kielektroniki ziwasaidie

kuingia tena uwanjani kwa kila mmoja kukaa eneo lilelile alilokata awali kwenye mchezo wa marudiano," inaeleza.

Inaeleza kuwa pia mfumo wa N-Card uruhusu kuuzwa tiketi zaidi kwa mashabiki wapya watakaoamua kuingia uwanjani siku hiyo hadi kufikia au kukidhi idadi inayoruhusiwa kulingana na uwezo wa uwanja

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwepo sintofahamu na kutokuaminiana kati ya baadhi ya klabu hususani Yanga na TFF kuendelea licha ya vikao vya kuiondoa sintofahamu hiyo, hivyo waziri ameahidi kuitisha kikao kingine haraka kati ya pande hizo mbili ili kujadili changamoto na kuondoa jakamoyo iliyopo.