Mgunda aanza na hesabu kali, mechi sita za heshima zatajwa

KOCHA Juma Mgunda ana siku 29 za kibabe na ngumu kwelikweli, lakini zikiwa ni za kimkakati na kama atatoboa itampa heshima kubwa mbele ya mashabiki wa Simba na wapenzi wa soka kwa ujumla nchini.

Ndio, Mgunda na kikosi cha Simba kinaanza kuhesabu siku hizo za kimkakati kuanzia leo wakati watakapoikaribisha Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku, huku wakijua ni ushindi tu utakaosaidia kurahisisha kupanda mlima mrefu ulio mbele yao.

Mchezo huo wa Dodoma, ni mwanzo wa ratiba ngumu inayoikabili Simba ndani ya Oktoba na kama Mgunda na jeshi lake watazichanga vyema karata inaweza kuwa na neema kwao lakini wakishindwa kufanya hivyo, huenda ikavuruga malengo waliyojiwekea msimu huu.

Kama hujui siku tano baada ya mchi hii ya Ligi Kuu Bara, Simba itakuwa na kibarua cha mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikisafiri hadi Angola na kucheza Jumapili ijayokisha wiki moja baadaye itarudiana nao kwenye Uwanja wa Mkapa, Oktoba 16.

Oktoba 23 itakabiliana na Yanga katika Dabi ya Kariakoo na siku nne baadaye itaumana na Azam, michezo yote ikiwa ni ya Ligi Kuu kama ambavyo itavyokabiliana pia Mtibwa Sugar, Oktoba 30 ukiwa ni wa kufungia pazia la mwezi huu. Kwa Mgunda anayekaimu nafasi ya kocha mkuu wa Simba, ushindi dhidi ya Dodoma leo utakuwa ni mwendelezo wa kufanya vizuri tangu alipopewa jukumu la kuiongoza mwezi uliopita ambapo chini yake imeibuka na ushindi mechi tatu, ikifunga mabao matano na kutoruhusu bao hta moja.

Ushindi wa leo, utaifanya Simba irejee kileleni mwa msimamo kwani itafikisha pointi 13 wakati kwa Dodoma Jiji, ikitakata itafikisha pointi nane na kupanda hadi nafasi ya tano. Dodoma iliyopoteza mechi mbili za mwanzo, itaikabili Simba ikiwa na hali nzuri ya kujiamini kutokana na mwenendo mzuri katika mechi tatu zilizofuatia dhidi ya Singida BS, Geita Gold na Kagera Sugar ikishinda mchezo mmoja na kutoka sare mbili huku ikiwa haijaruhusu bao lolote.

Kwa mujibu wa kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola, timu hiyo leo itawakosa wachezaji watatu kutokana na sababu tofauti huku akisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi leo.

“Tumepata siku mbili kwa ajili ya mechi yetu ya kesho (leo). Nasema Kwamba sio mechi rahisi kwa sababu Simba siku zote hatuna mechi rahisi. Ukiangalia Dodoma Jiji wameanza kwa kusuasua lakini mechi iliyopita wamepata matokeo. Lakini sisi tumejipanga kuhakikisha pamoja na ugumu wa mechi tunapata matokeo.”

“Kuna wachezaji tutawakosa. Mchezaji kama Shomari Kapombe ana majeraha lakini pia kuna Peter Banda ambaye alipata majeraha kule Zanzibar kwenye mechi za kirafiki na Pape Sakho mwenye matatizo ya kifamilia akiwa amepatwa na msiba,” alisema Matola.

Wageni Dodoma Jiji mbali ya kusaka pointi tatu katika mechi ya leo, ushindi utawafanya wamalize historia ya unyonge mbele ya Simba kwani imepoteza mechi zote nne walizokutana katika Ligi Kuu tangu walipopanda daraja.

Kocha msaidizi wa Dodoma, Mohamed Muya alisema wanajuan ugumu ulio mbele yao dhidi ya Simba lakini wamejiandaa kumaliza unyonge walionao mbele yao.

“Timu yetu tulianza vibaya lakini tukajipanga tuangalie tatizo liko wapi na tukaanza kubadilika kwenye matokeo. Tunakuja kucheza na Simba. Tunawaheshimu Simba, tunafahamu uwezo wao na uwekezaji wao lakini na sisi pia kwa jinsi tulivyojaliwa kusajili, tunaamini tuna timu ambayo inaweza kufiti kwenye daraja la ushindani.

“Tunakwenda kuendelea kutafuta ushindi kesho (leo). Sisi tunakwenda kupambana kesho ili tupate pointi tatu,” alisema Muya.

Mchezo mwingine leo utakuwa ni baina ya Mtibwa Sugar watakaoialika Mbeya City katika Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro kuanzia saa 10:00 jioni