Minziro, Wandiba tena Fountain Gate, Laizer ‘out’
Kocha Mkuu mpya wa Fountain Gate, Fredi Felix ‘Minziro’. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Minziro anaungana na msaidizi wake tena Mathias Wandiba baada ya kutofanya kazi kwa zaidi ya msimu mmoja, huku Laizer akipewa mkono wa kwaheri na Fountain Gate iliyopo nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 16 katika michezo 17.
Mbeya. Fountain Gate imethibitisha kuachana na Kocha wake Mohamed Laizer huku uongozi wa timu hiyo ukitangaza kumvuta kikosini Fredi Felix ‘Minziro’ kuiongoza timu hiyo kwa mechi zilizobaki za Ligi Kuu ya NBC.
Kwa hivi karibuni kumekuwapo na taarifa zisizo rasmi za Laizer kuachana na timu hiyo, ambapo leo Aprili 10, zimethibitishwa rasmi pande zote kukubaliana kuachana.
Minziro ambaye alikuwa Bigman ya Championship, anajiunga na timu hiyo akitarajia kusaidiana na Mathias Wandiba aliyekuwa akiiongoza Gunners nayo ya Championship kwa ajili ya kuiweka salama timu hiyo ya Ligi Kuu.
Wawili hao wanakutana kwa mara nyingine baada ya kuachana kwa takribani msimu mmoja tangu walipofanya kazi pamoja katika kikosi cha Pamba Jiji ya Mwanza kabla ya kila mmoja kutafuta malisho yake.
Pia makocha hao walishafanya kazi katika kikosi cha Mbeya City kabla ya Wandiba kutimkia Geita Gold kisha kuibukia Pamba Jiji katika kikosi cha timu ya vijana (U20) ambapo Gunners waliamua kumvuta na sasa wanakutana tena.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa timu hiyo, umesema Minziro atakuwa Kocha Mkuu akisaidiana na Wandiba, huku Aboubakari Francis akibaki na majukumu yake ya kocha msaidizi na Henry Joseph akibaki kuwa kocha wa viungo kikosini humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uongozi unaamini kupitia uzoefu wa kocha huyo na staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, weledi na kujitolea kwa benchi hilo, timu itaimarika zaidi na kufikia malengo yake kwenye mashindano.
“Wakati huohuo tunathibitisha kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Laizer, Fountain Gate inamtakia kila la heri katika majukumu yake, tunaendelea kujidhatiti katika kujenga timu kuwa imara, ushidani na kuleta mafanikio kwa mashabiki na wadau wake,” imesema taarifa hiyo.
Minziro anatua kikosini humo akiwa ameiacha Bigman katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya Championship ikiwa na pointi 27, huku msaidizi wake akiiacha Gunners ikiwa nafasi ya 10 na pointi 23 baada ya michezo 21.