Refa wa fainali ya Morocco, Senegal atoswa Kombe la Dunia
Refa Jean-Jacques Ndala Ngambo kutoka DR Congo akiwa ameshikilia kadi ya njano mkononi wakati wa mechi ya fainali ya AFCON baina ya Morocco dhidi ya Senegal. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Idadi ya marefa 170 wameteuliwa kuchezesha Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Dar es Salaam. Refa aliyechezesha mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 baina ya Morocco na Senegal, Jean-Jacques Ndala Ngambo kutoka DR Congo amekosa fursa ya kuchezesha Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu baada ya kutoteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Katika orodha ya marefa 170 ambayo imetolewa na FIFA, Ngambo sio mmojawapo licha ya miezi mitatu tu iliyopita kuchezesha fainali ya AFCON ambayo Morocco ilifungwa bao 1-0 na Senegal.
Hata hivyo mechi hiyo imeibua mgogoro mkubwa katika soka la Afrika ambao chanzo chake ni uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuamua kuivua ubingwa Senegal na kuitangaza Morocco kuwa bingwa kwa ushindi wa mezani wa mabao 3-0.
Uamuzi huo ulitokana na kile kilichotajwa na kamati hiyo kwamba Senegal waligomea mchezo licha ya kwamba baadaye uliendelea jambo kwa uamuzi wa refa Ndala.
Na kwa sasa wengi wamekuwa wakimlaumu refa Ndala kuwa chanzo cha mgogoro huo kwa kitendo chake cha kuruhusu mchezo uendelee jambo ambalo linawapa nguvu Senegal ya kuamini hawakuvunja kanuni.
Marefa saba wa kati kutoka Afrika wamepata fursa ya kuteuliwa kuchezesha Fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwaka huu kati ya 170 waliopata fursa hiyo.
Walioteuliwa ni Pierre Atcho (Gabon), Dahane Beida (Mauritania), Mustapha Ghorbal (Algeria), Jalal Jiyed (Morocco), Amin Mohamed (Misri), Tom Abongile (Afrika Kusini) na Omar Artan (Somalia).
Marefa wasaidizi ni Amos Abeigne na Boris Ditsoga (Gabon), Mahmoud Abouelrega na Ahmed Taha (Misri), Mustafa Akarkad na Zakaria Brinsi (Morocco), Mokrane Gourari (Algeria) na Santos Jerson wa Angola.
Marefa wa VAR ni Mahmoud Ashour (Misri) na Hamza El Fariq wa Morocco.