Motsepe asisitiza AFCON 2027 kupigwa Afrika Mashariki
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Fainali za AFCON 2027 zitashirikisha idadi ya timu za taifa 28 barani Afrika.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe amesisitiza kwamba Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitachezwa katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
Motsepe ametoa msisitizo huo jana Alhamisi, Aprili 9, 2026 katika ziara yake nchini Morocco.
Motsepe amesema kuwa haoni kitakachozuia Fainali hizo kuchezwa katika nchi hizo tatu mwakani na anaamini zitakuwa za aina yake.
“Ndio maana nilipeleka Kamati ya Utendaji ya CAF nchini Tanzania kuonyesha imani yangu kwa ukanda huo.
“Tutafanya kazi pamoja kuendeleza mpira wa miguu Afrika Mashariki na bara la Afrika kiujumla.
“Sina wasiwasi akilini mwangu kwamba tufanikiwa kuifanya AFCON 2027 ndani ya Kenya, Uganda na Tanzania kuwa ya mafanikio,” amesema Motsepe.
Msisitizo wa Motsepe umekuja katika kipindi ambacho nchi hizo tatu zimekuwa na wasiwasi wa kupoteza uenyeji wa mashindano hayo kutokana na kile kilichotajwa kuwa kutokidhi vigezo vya miundombinu na viwanja.
Fainali za AFCON 2027 kwa mara ya kwanza zitaandaliwa na nchi tatu lakini pia zitashirikisha idadi ya timu 28.