Mkataba wa Saido Simba kufuru

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Saido Ntibazonkiza kabla ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu kuitumia timu hiyo kulikuwa na masharti kwa upande wake na uongozi kila mmoja akiweka wazi kile anachohitaji.


Saido amekubali kufuata ratiba ya timu ikiwemo kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo husika kama ilivyo kwa wachezaji wengine jambo ambalo awali hakuwa anakubaliana nalo.


Awali Saido alikuwa anahitaji baada ya kucheza mechi au kutoka kwenye mazoezi awe anakwenda nyumbani tofauti na wachezaji wengine ambao wamekuwa wakirudi kambini na hata siku ya mechi haswa zile za hapa, Dar es Salaam awe anatokea nyumbani kwake.

Uongozi wa Simba ukiwakilishwa na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Abdallah 'Try Again' haukukubaliana na suala hilo kwani lingeweza kuwagawa wachezaji na mwisho wa siku Saido alikubali kufuata kama vile ambavyo ratiba ya timu itakuwa.


Baada ya hapo awali Saido alikuwa anataka mshahara USD 8000, zaidi ya Sh16 milioni ila Simba ilimshusha hadi USD 4000, zaidi ya Sh8 milioni na alikubali kuchukua ingawa kulikuwa na mvutano mkubwa katika eneo hilo.


Mvutano mwingine kati ya uongozi wa Simba na Saido ulikuwa kwenye pesa ya usajili mchezaji huyo alikuwa anataka Sh70 milioni ila mwisho wa siku pande zote mbili zilikubaliana na alichukua USD 30,000 zaidi ya Sh60 milioni kwa pesa ya Kitanzania.


Kwenye mkataba huo wa Simba kuna vipengele tofauti vinavyombana Saido kufanya masuala yoyote ya nidhamu kwani ikitokea jambo kama hilo kuna kiasi cha fedha kama faini atakuwa anakatwa kwenye mshahara wake kila mwisho wa mwezi.


Baada ya hapo uongozi wa Simba ulikubali sharti ya Saido kutaka kupewa nyumba nzuri ya kuishi wakati wote ambao atakuwa anaitumikia timu hiyo maeneo ya Masaki, Mikocheni na Oysterbay na haraka imeanza kutafutwa.