Morrison afungiwa mechi tatu, kuikosa Simba

WINGA wa Yanga, Bernard Morrison amelimwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda ambaye alikuwa ameanguka chini wakati wa harakati za kugombea mpira.

Morrison alifanya kosa hilo, mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapana kifungo kilichotumika kumuadhibu ni kanuni ya 42:5 (5.6) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa wachezaji, ambapo hatacheza dhidi ya Ruvu Shooting, Namungo FC na Simba.

Wakati Morrison akipata adhabu hiyo, waamuzi waliyosimamia mchezo huo (Yanga vs Azam), Ahmed Aragija, mwamuzi msaidizi namba moja Frank Komba kutoka mkoa wa Dra es Salaam, wamepelekwa kwenye kamati ya waamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwa ajili ya kujadiliwa baada ya kushindwa kuumudu vyema mchezo huo.


PRISONS vs SIMBA
Mwamuzi msaidizi namba mbili kwenye mchezo wa  Prisons na Simba, Black Tubuke kutoka mkoani Njombe amepelekwa kamati ya waamuzi ya TFF baada ya kuonekana kushindwa kumsaidia vyema mwamuzi wa kati mchezo huo.

Adhabu nyingine imekwenda kwa Geita Gold na Kagera Sugar, ambazo zimetozwa Shilingi 1milioni kwa kila moja kwa kosa la kuchelewa kutoka kwenye vyumba vya kuvalia nguo, hivyo mechi ilichelewa kuanza kwa dakika nne, adhabu hiyo imezingatia kanuni ya 17 (15 na 60) ya Ligi Kuu kuhusu utaratibu za mchezo.

Kwa mujibu wa kikao kilichofanyika Septemba 21 cha kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ilipitia muenendo na matukio mbalimbali ya ligi na kufanya maamuzi hayo na ilisisitiza klabu kuheshimu taratibu za michezo pamoja na haki za wadhamini wa matangazo.

Meneja wa vifaa wa  Kagera Sugar, Ramadhan Khalid amefungiwa mechi tatu kwa kukosa la kupinga maamuzi ya mwamuzi katika mechi yao na Geita Gold ambapo alichukua kiti na kukipiga chini dakika ya 77, wakati huo huo mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo, Ludovic Charles kapelekwa kwenye kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi, ili ajadiliwe baada ya kushindwa kumsaidia mwamuzi wa kati.
Kwa upande wa klabu ya Ruvu Shooting imetozwa faini ya Sh 3 milioni kwa kosa la kushindwa kuweka mabango ya wadhamini wake binafsi, Uwanja wa Uhuru wakati wa mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania, kinyume na matakwa ya kanuni 16:1 (1.5) ya ligi kuu kuhusu udhamini.

Mwamuzi wa kati kwenye mchezo wa Namungo na Coastal Union, Amina Kyondo kutoka Morogoro, kapelekwa kwenye kamati ya waamuzi ya TFF kwa ajili ya kujadiliwa kutokana na kuumudu vyema mchezo huo.
Wakati mchezaji wa Dodoma Jiji, Rajabu Habib amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Shilingi 500, 000 kwa kosa la kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina, wakati wa kupasha moto misuri, alionekana ameshika kitu mkononi ambapo alienda nacho golini akalizunguka mara kadha kisha akatupa chini na kukikanyaga kwa mguu.