Morrison atuliza presha Simba

Friday February 19 2021
simbapic

Benard Morrison

By Thobias Sebastian

Mara. Bao pekee la kipindi cha kwanza la winga, Benard Morrison lilitosha kuipa ushindi Simba na kufikisha pointi 42, nne nyuma ya vinara wa Ligi Kuu, Yanga.

Simba, ambayo bado ina faida ya michezo miwili mkononi, ilikuwa na mchezo mgumu mbele ya Biashara United, ambayo ilikubai kipigo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume, mkoani Mara.

Akituliza pasi ndefu kutoka wingi ya kushoto, kiungo huyo raia wa Ghana, alituliza vizuri kabla ya kumchagua kipa wa Biashara dakika ya 21 na kufanya mchezo huo kuwa mgumu kwa wenyeji.

Kocha wa Simba Didier Gomes Da Rosa alimtumia Meddie Kagere katika eneo la ushambuliaji kama mshambuliaji pekee aliyekuwa akisaidiwa na Perfect Chikwende na Morrison kwa pembeni, huku katikati kukiwa na Mzamiru Yassin na Thedeo Lwanga.

kocha huyo pia aliamua kuwapumzisha Clatous Chama na Luis Miquessone, kabla ya kuamua kumwingiza kiungo fundi wa Zambia, Chama dakika za mwisho kutokana na kuumia kwa Morrison.

Mchezo huo ulikuwa muhimu kwa Simba kutokana na kutaka kusogea kileleni, lakini pia kuinua ari wakijiandaa na mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Advertisement

Mchezo huo wa Kundi A la mashindano hayo makubwa zaidi Afrika katika ngazi ya klabu utafanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumanne, wakiwa wote wana pointi tatu na kuwania nafasi ya kupanda kileleni mwa msimamo.

Akizngumza baada ya mchezo wa jana, Da Rosa alisema ilikuwa muhimu kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kutokana na kuhitaji pointi tatu za kusogea kileleni mwa Ligi Kuu, lakini pia kuongeza morali kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Al Ahly.

“Tuna malengo pia na mashindano haya (Ligi Kuu Tanzania Bara), ndiyo maana tunaweka nguvu kote, lakini pia ushindi huu unaleta hali nzuri kambini wakati wa kuisubiri Al Ahly.

“Tunajua kuwa tunatakiwa kuwa bora kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya miamba hii ya soka, hivyo tunahitaji kuwa na kila kitu tayari uwanjani,” alisema kocha huyo raia wa Ufaransa.

Simba ambayo ilishinda ugenini dhidi ya AS Vita katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa kwa bao 1-0, inatarajia kurwejea Dar es Salaam leo kwa ajili ya mchezo huo wa kimataifa.

Kwa upande wake, Kocha wa Biashara, Francis Baraza alisema vijana wake walikuwa na mchezo mgumu nyumbani wa kutafuta pointi tatu lakini walikosa bahati katika nafasi zao chache.

“Hatukuwa na bahati naweza kusema, tulijiandaa kwa ajili ya mchezo huu, tunajua kuwa ulikuwa mgumu kwani mechi ya kwanza kule Dar es Salaam tulifungwa zaidi, hivyo tulikuwa tukicheza kwa tahadhari,” alisema Baraza.


Rais wa ZFF ajiuzulu

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Seif Kombo Pandu amejiuzulu.

Katika barua yake ambayo aliiandika juzi, inaeleza kuwa ameamua kujuuzulu nafasi hiyo kwa hiari yake bila ya kushurutishwa na mtu yoyote.

Alieleza kuwa sababu ya kujiuzulu katika nafasi hiyo ni kwa maslahi mapana ya nchi na mpira wa miguu kwa ujumla.

Nyongeza na Mosi Abdallah

Advertisement