Mtasingwa aingia na mguu wa bahati Kaizer Chiefs
Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Adolf Mtasingwa, ameanza maisha yake ndani ya Kaizer Chiefs kwa mafanikio baada ya kutwaa taji la Toyota Cup, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa wa Zimbabwe, Scottland FC, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Royal Bafokeng, Rustenburg nchini Afrika Kusini.
Mtasingwa, aliyesajiliwa na Amakhosi hivi karibuni, alipewa nafasi ya kuanza moja kwa moja katika kikosi cha kwanza na kocha mpya Fernando Da Cruz, akicheza sambamba na Lebohang Maboe katikati ya uwanja.
Licha ya kuwa ilikuwa mechi yake ya kwanza akiwa na Chiefs, Mtasingwa alionyesha utulivu mkubwa kwa kucheza pasi rahisi zisizo na makosa, akisaidia timu kutawala eneo la kiungo huku pia akishinda mapambano kadhaa dhidi ya viungo wa Scottland FC.
Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Mfundo Vilakazi dakika ya 17 baada ya kutumia makosa ya safu ya ulinzi ya Scottland kushindwa kuondoa mpira uliotokana na pasi ndefu ya Inacio Miguel, kisha kumshinda kipa Talbert Shumba.
Katika kipindi cha kwanza, Chiefs walionekana kuwa na ubora mkubwa kupitia Vilakazi, Asanele Velebayi na Ethan Chislett, huku Mtasingwa akitimiza majukumu yake ya kulinda safu ya kiungo na kuanzisha mashambulizi kwa utulivu.
Scottland FC walijaribu kurejea mchezoni kipindi cha pili baada ya kumuingiza nyota wao Knowledge Musona pamoja na Khama Billiat, ambao wote waliwahi kuichezea Kaizer Chiefs, lakini safu ya ulinzi ya Amakhosi ilibaki imara na kuwazuia wapinzani wao kutengeneza nafasi nyingi za hatari.
Kocha Da Cruz pia aliwapa nafasi Wandile Duba, Luke Baartman na Sibongiseni Mthethwa, huku Duba akishindwa kutumia baadhi ya nafasi alizopata kuongeza mabao.
Bao la Vilakazi lilitosha kuipa Kaizer Chiefs ushindi wa kwanza wa Toyota Cup katika historia yao, baada ya kupoteza fainali mbili zilizopita dhidi ya Yanga ya Tanzania na Asante Kotoko ya Ghana.
Kwa Mtasingwa aliyevaa jezi namba 22, ushindi huo ni mwanzo mzuri wa safari yake ndani ya klabu hiyo kubwa ya Afrika Kusini, huku kiwango alichokionyesha katika mechi yake ya kwanza kikitoa matumaini makubwa kwa mashabiki wa Amakhosi kuelekea msimu wa 2026-2027.