Mtibwa, Kagera wafanya Ligi Kuu kijiwe

Muktasari:

Kwa zaidi ya miaka 12 ambayo timu hizo zimeshiriki kwenye ligi hiyo, zimeshindwa kuchukua ubingwa wala kutoshuka daraja.

Dar es Salaam. Timu za JKT Ruvu, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zimeigeuza Ligi Kuu Tanzania Bara kama kijiwe cha kupotezea muda kutokana na kutonufaika wala kunufaika na ligi hiyo.

Kwa zaidi ya miaka 12 ambayo timu hizo zimeshiriki kwenye ligi hiyo, zimeshindwa kuchukua ubingwa wala kutoshuka daraja.

Mbali na kutotwaa ubingwa, timu hizo tatu zimeshindwa hata kumaliza kwenye nafasi mbili za juu na ndani ya kipindi cha misimu 12 mfululizo ya ligi hiyo, zikizidiwa hata na Azam iliyopanda Ligi Kuu mwaka 2008.

Mtibwa iliyopanda Ligi Kuu mwaka 1996, imeshindwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo tangu mwaka 2000 ilipotetea taji lake ililolibeba mwaka 1999 na tangu hapo imekuwa ikishiriki bila kumaliza kwenye nafasi mbili za juu wala kushuka daraja.

Ruvu JKT nayo tangu ilipoanza kushiriki ligi hiyo mwaka 2002 imekuwa kama mshiriki tu kwani haijawahi kutwaa ubingwa, kumaliza kwenye nafasi mbili za juu pia haijawahi kushuka daraja licha ya kuponea chupuchupu kufanya hivyo mara kadhaa.

Kama ilivyo kwa JKT Ruvu, Kagera Sugar nao hawajawahi kushuka tangu miaka ya 90 wakati huo ikiitwa Kagera Stars, lakini licha ya mwanzoni mwa miaka ya 2000 kuanza kudhaminiwa na Kiwanda cha Sukari cha Kagera, mafanikio pekee ambayo imewahi kuyapata, ni kushika nafasi ya nne.

Ukiondoa timu hizo tatu, timu za Prisons, Ruvu Shooting, Toto Africans na Majimaji zimekuwa na homa za vipindi kwa kushuka daraja baadhi ya nyakati na kupanda, ingawa nazo zimekuwa hazina mafanikio yoyote ya kujivunia.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema kuwa nguvu ya fedha wanazotumia Simba, Yanga na Azam ndiyo inasababisha timu nyingine kucheza kubaki ligi si bila ubingwa. “Sisi wengine ni tofauti na Simba, Yanga na Azam huwa tunacheza mpira kwa nguvu ndani ya uwanja wetu, lakini wao hutumia sana nguvu ya fedha nje ya uwanja kuhakikisha wanapata ushindi na zaidi kuweka kambi za nguvu na kuandaa wachezaji.

“Katika hali kama hiyo ni ngumu kwa timu zetu kushindana nazo lakini madhara yake ni kuwa pindi wanapokwenda kushiriki mashindano ya kimataifa huwa hawafiki kokote,” alisema Maxime.

Kaimu kocha mkuu wa Mtibwa, Zubeiry Katwila aliunga mkono hoja ya Maxime akidai kuwa timu nyingine zimekuwa zikiangushwa na bajeti kiduchu kulinganisha na timu za Simba, Azam na Yanga.

“Timu kama Mtibwa kila msimu inaondokewa na wachezaji wazuri ambao hupewa fedha nyingi zaidi kwenye hizo timu zinazoitwa kubwa. Inakuwa ni vigumu kumzuia mchezaji kwa sababu soka ni maisha yake na huko anakokwenda anapata fedha nyingi zaidi.

“Hivyo tunajikuta kila msimu tunakuwa na kazi ya kuanza upya kutengeneza timu lakini kama tungekuwa na uwezo wa kuwafanya wachezaji wabaki, nadhani tungekuwa tishio,” alisema Katwila.

Aliyewahi kuwa kocha wa Prisons, Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema kuwa timu ndogo hazifanyi vizuri kwa sababu TFF huzipa kipaumbele timu kubwa za Yanga, Simba na Azam.

“Ukiangalia kwa mfano namna ya ratiba ya ligi inavyoandaliwa, kipaumbele cha kwanza huwa kwa Simba, Azam na Yanga. Zenyewe zinapewa muda mwingi wa kupumzika na kujiandaa kwa mechi tofauti na timu nyingine...zinapokwenda kucheza mikoani, hupangiwa ratiba ya kuziwezesha kumaliza mechi zote za ukanda au mkoa husika. “Kwa timu nyingine inaweza kupangiwa mechi mkoa fulani, mechi inayofuata ikatakiwa kurudi uwanja wa nyumbani halafu mechi ya tatu ikapangwa tena kucheza mkoa ule ambako ilicheza mechi ya mwanzo. Hapo timu zinakosa muda wa kupumzika na ndio maana hazifanyi vizuri,” alisema Meja Mingange.