Mtibwa Sugar ni ubingwa au tatu bora Ligi Kuu
Muktasari:
- Mtibwa Sugar ndio timu pekee tofauti na Simba au Yanga iliyowahi kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zaidi ya mara moja.
Mtibwa Sugar imetamba kuwa lengo lake kuu katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/2026 ni kutwaa ubingwa na kama ikishindwa kufanya hivyo basi imalize katika nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa ligi.
Ofisa habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema kuwa kucheza Ligi ya Championship msimu uliopita kumewapa somo hivyo hawako tayari kurudia makosa msimu ujao na badala yake wanataka kumaliza juu jambo ambalo amesema wana historia nalo.
"Naamini Mtibwa hatutawaangusha mashabiki wetu. Tunataka kuingia kwenye tatu bora au kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC. Tumewahi kufanya hivyo mara mbili ambazo ni 1999 na 2000.
"Tumerejea rasmi nyumbani kwa ajili ya msimu wa ligi ambao unaanza Septemba 16. Tumekuwa kwenye matayarisho kwa takribani wiki ya nne sasa. Lengo ni kurejea kwa kasi katika msimu ujao.
“Tumefanya usajili mzuri. Tumeleta mwalimu mzuri sana. Na tunaamini Mtibwa Sugaf hatutowaangusha Watanzania na mashabiki wetu. Wametusapoti sana tulipokuwa Ligi ya Championship," amesema Kifaru.
Kifaru ametamba kuwa wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanamudu ushindani wa ligi na amewataka mashabiki kukaa mkao wa kula.
"Tutaonyesha mazuri yetu ili kuwapa furaha wale wote waliokuwa wanatusapoti. Ligi sio lelemama msimu ujao na sisi Mtibwa Sugar tumejipanga vyema. Na matumaini ni makubwa sana msimu unaokuja.
"Tunatamani kupeleka furaha kubwa nyumbani msimu huu. Tutaonyesha mazuri yetu kuwapa furaha wale ambao walionyesha kutunga mkono msimu uliopita. Tumeweka kambi nyumbani kwenye mashamba yetu ya miwa.
“Matumaini ni makubwa sana ya kung’ara. Klabu zimefanya usajili mzuri na zina walimu wazuri lakini Mtibwa Sugar tunatamani kufanya vizuri,” amesema Kifaru.