Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtoto wa Rio Ferdinand ajiunga na Brighton

Muktasari:

  • Akiwa golikipa, Lorenz ameonyesha maendeleo ya haraka na tayari ameshiriki mchezo wake wa kwanza katika mashindano ya Premier League 2 mwaka huu

London, England. Lorenz Ferdinand, mtoto wa kwanza wa nguli wa zamani wa Manchester United Rio Ferdinand, amejiunga rasmi na klabu ya Ligi Kuu ya England baada ya kuhitimu kutoka akademia ya vijana ya Brighton na kujiunga na timu kubwa.

Lorenz mwenye umri wa miaka 18, ambaye ni mtoto wa marehemu Rebecca Ellison, mke wa kwanza wa Rio, alianza safari yake ya soka akiwa sehemu ya kikosi cha vijana wa chini ya miaka 13 cha Brighton, maarufu kama “The Seagulls.”

Akiwa golikipa, Lorenz ameonyesha maendeleo ya haraka na tayari ameshiriki mchezo wake wa kwanza katika mashindano ya Premier League 2 mwaka huu. Ili kupata uzoefu zaidi wa uchezaji, alipelekwa kwa mkopo katika klabu ya Havant & Waterlooville iliyoko ligi ya chini, baada ya kipa wa kwanza wa timu hiyo, Ben Dudzinski, kuumia na kutokuwa sehemu ya kikosi kilichosalia mwaka jana.

Akiwa na Havant & Waterlooville, Lorenz alicheza mechi sita bila kupoteza huku mbili akicheza bila kuruhusu goli, akionyesha kiwango cha kuvutia.

Lorenz ni mmoja wa wachezaji 13 waliotoka katika akademia ya Brighton na kusaini mikataba timu hiyo inayoongozwa na kocha Fabian Hurzeler. Wengine waliopata nafasi hiyo ni pamoja na Harry Howell na Freddie Simmonds, ambao tayari wamewahi kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza.


Mkurugenzi wa akademia ya Brighton, Ian Buckman, amesema:

"Tunafurahi kuwaona vijana hawa wakisaini mikataba yao ya kwanza. Wengi wao wamekuwa nasi tangu wakiwa na umri mdogo na tayari wamepata uzoefu wa kucheza na kikosi cha chini ya miaka 21, huku baadhi wakihusishwa na kikosi cha kwanza. Tunatarajia kuwaona wakikua zaidi na kuchangia mafanikio ya klabu kwa miaka ijayo."

Lorenz sasa anaungana na kundi la vijana wengine wa mastaa wa zamani wa Ligi Kuu ambao wanafuata nyayo za baba zao ambao ni pamoja na  Kai Rooney (15), mtoto wa nahodha wa zamani wa England Wayne Rooney, anayeng’ara katika akademia ya Manchester United, pamoja na Jaden (18) na Reigan Heskey (16), watoto wa Emile Heskey, wanaochezea kikosi cha vijana cha Manchester City.

Wachezaji hawa wana ndoto ya kufuata nyayo za vijana kama Jayden Danns, mtoto wa nyota wa zamani wa Liverpool Neil Danns, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza na Liverpool msimu uliopita.

Pia makinda hawa wanaweza kufikia mafanikio ya Liam Delap, mtoto wa Rory Delap wa Stoke City, ambaye msimu huu amesajiliwa na Chelsea kwa dau la pauni 30 milioni baada ya kung’ara katika Ligi Kuu akiwa na Ipswich.

Mkataba huu mpya kwa Lorenz unakuja mwaka mmoja tu tangu ajiunge na kampuni ya usimamizi wa wachezaji ya New Era Sports Management, ambayo pia inawakilisha wachezaji kama Michael Keane (Everton), Mason Holgate, Ollie Palmer (Wrexham) na Ben Godfrey (Atalanta).

Lorenz ni sehemu ya kizazi kipya cha watoto wa nyota wa zamani wa Ligi Kuu ya England wanaolenga kutengeneza majina yao katika soka la juu, wakifuata nyayo za baba zao.