Prime
Mzize na bahati isiyojirudia mara mbili
Muktasari:
- Msimu uliopita Mzize alihusika katika mabao 19 ambapo alifunga 14 na kutoa pasi tano za mabao
Dar es Salaam. Siku chache zilizopita Klabu ya Yanga ilitangaza taarifa ya mshambuliaji wao Clement Mzize kwamba atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa takribani wiki nane hadi 10 kutokana na kufanyiwa upasuaji wa sehemu ya goti baada ya kupata jeraha hilo Septemba 19, 2025 katika mechi ya hatua ya awali raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilipokuwa ugenini dhidi ya Wiliete ya Angola.
Nyota huyo ambaye alipandishwa kwenye kikosi cha wakubwa akitokea timu ya vijana alionyesha makali yake katika kufumania nyavu za timu pinzani na msimu uliopita wa 2024-2025 ulikuwa wa neema kwake baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu ndani ya kikosi cha Wananchi.
Msimu uliopita Mzize alihusika katika mabao 19 ambapo alifunga 14 na kutoa pasi tano za mabao huku akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyefunga mabao mengi akifuatiwa na Nassor Saadun wa Azam FC aliyefunga mabao nane sawa na Paul Peter wa Dodoma Jiji.
Ukiachana na Ligi Kuu ya NBC ambayo aliisaidia Yanga kubeba taji lake la nne mfululizo, mshambuliaji huyo aling’ara pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga ilishiriki katika hatua ya makundi.
Katika hatua hiyo Mzize aliisaidia Yanga kupata pointi tatu muhimu katika mechi dhidi ya TP Mazembe ambayo ilipigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo Yanga ilitoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 3-1 baada ya wapinzani wao hao kutokea DR Congo kutangulia kwa bao moja katika dakika za mwanzoni mwa mchezo bao ambalo lilifungwa na golikipa, Alioune Faty kwa mkwaju wa penalti.
Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika Mzize aliifungia Yanga bao la kusawazisha ambalo alifunga kwa kupiga shuti kali kutokea umbali mrefu huku bao hilo likichaguliwa kuwa bao bora la wiki la CAF. Katika mechi hiyo nyota huyo alifunga mabao mawili lingine akifunga kipindi cha pili katika dakika ya 60.
OFA ZIKAANZA KUTUA
Baada ya kuonyesha kiwango bora katika msimu uliopita Klabu ya Yanga ilianza kupokea ofa nono kutoka katika Vilabu tofauti vya ndani na nje ya Bara la Afrika vikihitaji huduma ya Mzize.
Awali mchezaji huyo alihusishwa na klabu kutoka Ubelgiji, Misri, Afrika Kusini na Morocco kabla ya kuibuka taarifa ya ofa nyingine kutoka Qatar.
ESPERANCE
Kwa upande wa Watunisia hao, iliripotiwa kwamba walikuwa tayari kutoa Dola 1 milioni (zaidi ya Sh2 bilioni) kiasi ambacho awali Yanga ndicho ilikitaja ili kumuachia Mzize.
AL ETTIHAD
Al Ettihad ya Libya ilituma ofa ya takribani Sh3 bilioni ili kumchomoa pale Jangwani dili ambalo lilionekana kama lingefanikiwa lingevunja rekodi za sajili kubwa za wachezaji wa ndani kuwahi kufanyika katika soka la Tanzania ukiachana na usajili wa Mbwana Samatta ambaye alisajiliwa na TP Mazembe kwa Sh250 milioni mwaka 2011 na baadaye akauzwa kwa Sh2.1 bilioni kwenda KRC Genk ya Ubeligiji mwaka 2016.
UMM SALAL
Klabu hii ya Qatar, nayo iliripotiwa kuitaka saini ya Mzize ikitoa ofa ya Dola 900,000 (zaidi ya Sh2.2 bilioni) pamoja na kumpa mshambuliaji huyo mshahara wa Dola 20,000 (Sh50 milioni) kwa mwezi.
AL ASAD
Kutoka Qatar, klabu hii nayo ilitajwa kuiwania saini ya Mzize na mezani ikiwa na ofa ya Sh2 bilioni kama ilivyokuwa kwa Esperance.
YANGA ILIVYOFUNGA MJADALA
Agosti 2025, ikiwa ni takribani mwaka mmoja na siku kadhaa zimepita tangu Yanga itangaze dau la Mzize ni si chini ya Sh2 bilioni, uongozi wa klabu hiyo ulifunga mjadala kwa kutamka hadharani kwamba mshambuliaji huyo ataendelea kuutumikia mkataba wake wa miaka miwili hadi 2027, hivyo hakuna biashara itakayofanyika.
Taarifa hiyo alibainisha kuwa, sababu ya Yanga kufanya hivyo ni kwamba, uongozi umeona hauwezi kuruhusu kuwaachia wachezaji muhimu kwa wakati mmoja, hiyo ni baada ya kumuuza Stephane Aziz KI aliyesajiliwa na Wydad Casablanca ya Morocco.
BAHATI HAIJIRUDII MARA MBILI
Huenda Klabu ya Yanga isije kupokea tena ofa za mabilioni kwa nyota huyo wa Taifa Stars kwani kuwa kwakwe nje ya Uwanja kwa wiki nane hadi 10 ambazo ni takribani na miezi miwili nusu ni dhahiri kabisa hatoweza kufikia kiwango alichokionesha katika msimu uliopita na pengine thamani yake ikashuka zaidi katika soko la usajili.
Ndani ya hizo wiki nane mpaka 10 ambazo atakosekana kwenye kikosi cha Yanga ambacho kwa sasa kinaongozwa na kocha Mreno, Pedro Gonçalves, mshambuliaji huyo ataikosa michezo kadhaa ikiwemo miwili ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria wakati katika Ligi Kuu ya NBC miongoni mwa michezo atakayoikosa ni pamoja na ule wa Dabi ya Kariakoo utakaopigwa Desemba 13, 2025.
Pia kuna uwezekano mkubwa Mzize akazikosa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Mshambuliaji huyo ambaye ni miongoni mwa wachezaji nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' tayari ameshakosa mechi mbili zilizopita za timu hiyo na sasa anaelekea kuzikosa fainali za AFCON 2025 ambazo zitafanyika Morocco kuanzia Desemba 21 mwaka huu hadi Januari 18 mwakani.
Wakati Mzize akitarajiwa kuwa nje kwa muda usiopungua wiki nane, zimebaki wiki saba tu kabla ya kuanza kwa fainali za AFCON 2025 ambazo Taifa Stars itakuwa katika kundi C pamoja na timu za Tunisia, Uganda na Nigeria.
Mzize ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika kikosi cha Taifa Stars ambacho amekuwa miongoni mwa nyota wanaocheza mara kwa mara.
Mshambuliaji huyo alithibitisha hilo katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) 2024 ambapo aliibuka mfungaji bora wa Taifa Stars baada ya kupachika mabao mawili.
Kukosekana kwakwe katika mashindano hayo makubwa Afrika hatopata fursa ya kuonyesha kiwango chake kama ilivyo kawaida kwa wachezaji wengine ambao hutumia mashindano makubwa kama AFCON kuzivutia timu mbalimbali katika usajili.