Nabi: Nini? kuna Aziz Ki

MASHABIKI wa Yanga bado wanakikumbuka kipigo walichopata Jumamosi iliyopita dhidi ya Vipers ya Uganda kwenye mchezo wao wa kirafiki, lakini unajua kinachowapa kiburi na hawana hofu. Hapa kuna Aziz Ki, pale Mayele.

Pamoja na kipigo hicho, Yanga wala haijatoka kwenye reli na wapinzani wajipange msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na itaanza na mtani wake Simba kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasredne Nabi alisema matokeo ya mchezo huo yamemwonyesha ni nini watakwenda kufanya kwa siku zilizobaki kabla ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa pande zote mbili kuona makali yao wakiukaribisha msimu mpya.

Nabi anaendelea kuwapika vijana wake kwenye kambi yao ya Avic, Kigamboni na anatarajia makubwa kutoka kwao akiwamo nyoa mpya Aziz Ki akiamini atawashangaza kwa kumfunga mtani Jumamosi, Agosti 13.

Mbali na Nabi, mastaa wa zamani wa timu hiyo wamekiangalia kikosi cha timu yao na licha ya matokeo yaliyopita ambayo wanaamini wapinzani wao watayachukulia kama Yanga haitatisha msimu ujao na kutamba uwepo wa Aziz Ki utaibeba na atawashangaza.


MOTO WA STAA WAO MPYA AZIZ KI

Wakimwelezea Ki kwa nyakati tofauti, mastaa wa zamani, beki Williams Mtendamema aliliambia Mwanaspoti Aziz Ki ni fundi atakayesaidiana na Mayele kuzalisha mabao mengi, isipokuwa kwa sasa anatakiwa kuyazoea mazingira kwa haraka.

Ki ambaye usajili wake ulitikisa Yanga ikimsajili kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast kiwango alichokionyesha dhidi ya Vipers ya Uganda ndicho kilichomfanya Mtendamema kumchambua kiufundi.

“Mashabiki wanapaswa kumpa muda, ni mchezaji mzuri sana, wasitarajie mechi moja tu anafanya makubwa, kuna kuzoea mazingira na bado kocha anatengeneza kombinesheni,” alisema na kuongeza;

“Wachezaji wa Yanga walionyesha uwezo wa mchezaji mmoja mmoja siyo kitimu walipocheza na Vipers lakini wengi wanajua mpira, ukiachana na Ki yupo Gael Bigirimana jamaa haimbwi ila atakuja kuwashangaza wengi.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Andrew Tito alisema kupitia tamasha la Wiki ya Mwananchi, ameona ufundi wa mastaa, anaamini baada ya mechi tatu za Ligi Kuu Bara ikianza Agosti 15 watafanya makubwa.

“Kikosi cha Yanga kina wachezaji watulivu wanaotumia akili kubwa, ukiachana na waliyokuwepo na timu msimu uliyoisha, hawa wapya wameongeza nguvu mfano Ki na Bigirimana,” alisema.