Nabi: Sure Boy atacheza hapa

KIUNGO Salum Abubakar ameanza mazoezi yake ya kwanza tu akiwa na Yanga yakatosha kwa kocha wake Nasreddine Nabi kutamka kauli zitakazozishtua wengi.

Nabi amelifungukia Mwanaspoti kuhusu usajili wa staa huyo maarufu kwa jina la Sure Boy kwamba kikosi chake kimepewa mtu sawa na Khalid Aucho.

Nabi alisema Sure Boy ni kiungo mzawa ambaye ana ubora kama wa Aucho katika kutekeleza majukumu eneo la kiungo na sasa kikosi chake kimekamilika sehemu hiyo.

“Nimefurahia sana usajili huu. Nimeangalia ubora wake hapa (mazoezini) amenionyesha kwamba ni mmoja kati ya wachezaji bora wa hapa Tanzania atakayetusaidia sana,” alisema Nabi.

“Kwa sasa unapomkosa Aucho unakuwa huna presha kwa sababu una mwingine (Sure Boy). Nafikiri tuko sawa eneo la kiungo, hatuna wasiwasi tena kama ilivyokuwa hapo kabla.”

Kocha huyo alifafanua kuwa Sure Boy anaweza kupiga pasi za aina zote fupi na ndefu, lakini pia akimudu kuhama nafasi moja kwenda nyingine katika kumiliki eneo la kiungo.

“Sure Boy anakaba vizuri, lakini pia ana ubora mkubwa katika kupiga pasi ndefu na zile fupi. Namuona anaweza kucheza eneo lote la kiungo hata tukiamua kumsogeza juu kidogo karibu na mshambuliaji wa mwisho.

“Kuna wakati mpira unaweza kuchezwa na viungo wengi na bado timu ikawa bora na kupata matokeo. Sure Boy ataongeza ushindani wa nafasi na kila mchezaji sasa ataongeza ubunifu ili aweze kupata nafasi.”


HUYU HAPA MWENYEWE

Akizungumza na Mwanaspoti, Sure Boy alisema licha ya Yanga kuwa na mastaa kibao eneo la kiungo, haogopi ushindani na anaamini ataingia kikosi cha kwanza.

Alisema mpira unachezwa uwanjani na amepanga kuonyesha kiwango bora mazoezini kisha Nabi ataamua nani amtumie.

Alisema hata wakati anaanza kucheza Azam 2007 alikutana wa mastaa bora kina Ramadhani Chombo ‘Rendondo’, Kipre Tcheche, Kipre Balou, Mrisho Ngassa, Mussa Mude na Jabir Azizi ‘Stima’ lakini alipenya na kuingia kikosi cha kwanza.

“Ambacho naamini kama nitafanya mazoezi vizuri na kufuata kile ambacho kocha anahitaji, basi nitapewa nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza. Naheshimu ubora wa kila mchezaji na anastahili kuwepo hapa, lakini nimekuja kuongeza kitu ili kufikia mafanikio msimu huu,” alisema.

“Yanga ni timu kubwa huwezi kusajiliwa mchezaji kama hauna kitu cha kuja kuongeza. Basi kama ambavyo wao waliniamini na kuona kitu kwangu, nitapambania na kuipigania klabu hii ili kufikia kile ambacho kila mmoja anatamani kukiona kutoka kwangu. Hivyo tusubiri muda ufike nadhani hiki ambacho nakizungumza wakati huu nitakwenda kukihamishia katika mechi zilizo mbele yetu.”


BADO STRAIKA

Kocha Nabi alisema mara baada ya usajili huo bado anatafuta straika mmoja atakayeziba nafasi ya Yacouba Songne (majeruhi), kipa na beki wa kati.

“Tunatakiwa kutafuta mtu sahihi wa pale ambapo Yacouba ameishia msimu huu, bado hatujapata mtu sahihi ndani ya timu. Kwa sasa kuna nguvu inapungua, lakini pia kuna kipa tunatakiwa kutafuta na beki wa kati,” alisema kocha huyo.

Yanga inamfukuzia kiungo mshambuliaji wa TP Mazembe, Chico Ushindi huku pia Mwanaspoti linafahamu yupo winga raia wa Mali anapigiwa hesabu na mmojawao atachukua nafasi wakitaka kusajili jina moja la staa wa kigeni dirisha dogo.

(IMEANDIKWA NA KHATIMU NAHEKA, THOBIAS SEBASTIAN NA OLIPA ASSA)