Nane kizimbani utata kifo cha Maradona

Muktasari:

  • WATU nane watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kifo cha mwanasoka nguli wa zamani wa timu ya taifa Argentina, Diego Maradona aliyefariki Dunia mwaka 2020.

LONDON, ENGLAND. WATU nane watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kifo cha mwanasoka nguli wa zamani wa timu ya taifa Argentina, Diego Maradona aliyefariki Dunia mwaka 2020.


Hatima ya maisha ya Maradona ilikuwa mikononi mwa madaktari wake waliokuwa wakimtibu, hata hivyo kulikuwa na mashaka kuhusu chanzo cha kifo chake.


Kwa mujibu wa taarifa endapo watu hao watakutwa na hatia, watapewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 25 jela kwa mujibu wa sheria.


Mashtaka yataanza kusikilizwa mwakani na itajumuisha jopo zima la madaktari, waliokuwa wakimtibu Maradona tangu alipoanza kuumwa kwa mujibu wa gazeti la AP News lililoripoti taarifa hiyo.


Aidha taarifa zimezidi kuripoti mawakili wa familia ya Maradona, wanapambana kuhakikisha watu wote waliyohusika na kifo cha Maradona, watakutwa na hatia.


Mawakili hao wamedai kifo cha Maradona, kimetokana na kitendo cha madaktari, kuamuacha peke yake hadi umati ulipomfika nyumbani kwake kwa mujibu wa taarifa.


Mkongwe aliyejitengenezea heshima Argentina na dunia kwa ujumla, alifariki dunia mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 60, baada ya kufanyiwa uporesheni ya ubongo.