Nidhamu yaibeba JKT mbele ya Yanga jeshini

Picha na Loveness Bernard

Muktasari:

  • Kwa mara ya pili msimu huu wa 2023/24, Yanga imetoka suluhu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, mara ya kwanza ilikuwa February 2 mwaka huu dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.

NIDHAMU nzuri ya kujilinda kwa vijana wa Malale Hamsini, JKT Tanzania ni miongoni mwa mambo ambayo yaliifanya Yanga kuwa na wakati mgumu kuifungua ngome ya maafande hao katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Kwa mara ya pili msimu huu wa 2023/24, Yanga imetoka suluhu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, mara ya kwanza ilikuwa February 2 mwaka huu dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Yanga iliuanza mchezo huo huku katika safu yake ya ushambuliaji ikiwa na Joseph Guede ambaye ameonakana kuwa katika kiwango bora kwa sasa huku akishirikiana na Kennedy Musonda na Augustine Okrah.
Huku nyuma yao akiwepo kinara wa mabao ligi kuu, Stephane

Aziz KI kwa kuiheshimu Yanga, kocha wa JKT Tanzania, Malale Hamsini aliingia na mpango wa kujilinda huku akishambulia kwa kustukiza.

Katika hilo kocha huyo alifanikiwa kutokana na idadi kubwa ya wachezaji ambao JKT ilikuwa nao ambao ni wachezaji nane kila ambapo Yanga ilikuwa ikifanya mashambulizi yake.
Mabeki wa JKT Tanzania, George Wawa, David Bryson, Edson Katanga na Issa Haidary ambao walikuwa wakiunda ukuta wao, walikuwa na wakati mzuri kimchezo huku wakiongozwa na kipa wao, Yakubu Suleiman.

Hata wale ambao walikuwa wakicheza pembeni, Wawa na Bryson ambaye alicheza dhidi ya waajiri wake wa zamani hakuna ambaye alikuwa akipandisha mashambulizi kazi hiyo waliwaachia mawinga wao, Sabilo na Kichuya ambao nao walisaidia kulinda.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ilimbidi kufanya mabadiliko ya haraka kwa kumtoa Okrah ambaye alionekana kuchemka huku akiingia Clement Mzize na kama ilikuwa haitoshi baadae akafanya tena mabadiliko mengine ikiwemo kuingia kwa Jonas Mkude, Farid Mussa  na Mwamnyeto.

Nyota hao waliingia kuchukua nafasi ya Nzengeli, Kibabage na Musonda. Mabadiliko ya JKT alijikita katika kuzuia jambo ambalo lilionekana kuwa na matunda katika mpango wao wa kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja.

Awali mechi hiyo ilipangwa kufanyika jana ila ilishindwa kuchezeka hivyo kuahirishwa na Kamishina wa mchezo, Kamwanga Tambwe kwa sababu ya hali ya uwanja huo kujaa maji sehemu ya kuchezea kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizi, Yanga ilishinda mabao 5-0, mechi iliyopigwa Agosti 29, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Mpia

Nzengeli aliyefunga mawili huku Stephane Aziz KI, Kennedy Musonda na Kouassi Yao wakifunga moja kila mmoja wao.
Tangu msimu wa 2018/2019, timu hizi zimekutana katika michezo minane ambapo kati ya hiyo Yanga Imeshinda sita huku miwili ikienda suluhu na mbali na ya leo ila sare ya kwanza baina yao ilikuwa ya bao 1-1, Juni 17, 2020.
Katika michezo hiyo, Yanga imefunga jumla ya mabao 16 huku JKT Tanzania ikifunga matatu.

JKT imeendeleza mwenendo mbovu wa matokeo kwani imefikisha michezo 14 mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, mechi iliyopigwa Uwanja wa Manungu Complex mjini Morogoro Novemba 3, mwaka jana.

Yanga imefikisha jumla ya pointi 59, katika michezo 22 iliyocheza hivyo kuhitaji pointi 15 tu ili kufikisha 74 na kutwaa ubingwa wake wa tatu mfululizo na wa 30 wa Ligi Kuu Bara kwa sababu hazitaweza kufikiwa na timu yoyote.

Iko hivi. Azam iliyoko ya pili na pointi 54 hata kama itashinda michezo yake sita iliyobaki itafikisha pointi 72 sawa na Simba inayoshika ya tatu na pointi 46 kwani ikishinda mechi zake zote tisa zilizobakia itaishia na pointi 73.

Kwa upande wa Maafande wa JKT, katika michezo yake 23 iliyocheza ya Ligi Kuu Bara hadi sasa imeshinda minne tu, sare 11 na kupoteza minane ikiwa nafasi ya 13 na pointi 23.

NDEMLA ATAKATA
Uwezo wa Said Ndemla katika upigaji wa mipira mirefu, uliifanya JKT Tanzania kusogea kwa haraka wakati wakisukuma mashambulizi yao kupitia maeneo yao ya pembeni ambayo walicheza, Shiza Kichuya na Sixtus Sabilo.
Pamoja na Yanga kuwa na Aucho katika eneo lake la  kiungo, Ndemla alionekana kuwa bora zaidi ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, alimudu pia kuwafungua kwa kupenya na mpira wakati ilipohitajika kufanya hivyo.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba, alikuwa akiwapa wakati mgumu Aucho na Nzengeli ambao walikuwa wakikumbana naye mara kwa mara katika eneo hilo, alitengeneza nafasi mbili na kunyang'anya mipira mara nne katika dakika 45 za kwanza.

Mchezaji huyo ambaye aliibeba JKT Tanzania katika eneo la kiungo alikuwa akishirikiana na Hassan Maulid 'Machezo' ambaye mara nyingi alionekana katika kuzuia kuliko kuchezesha timu.

NZENGELI AACHIWA KIUNGO
Licha ya kuwa na viungo halisi wa kati, Jonas Mkude na Zawadi Mauya katika kikosi chake, kocha wa Yanga, Miguel Gamond aliamua kuanza na winga, Max Nzengeli katika eneo hilo.
Tofauti na alivyozoeleka kucheza katika maeneo ya pembeni akiwa na Yanga, Nzengeli aliachiwa msala wa Mudathir Yahya ambaye hakuwa sehemu ya mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza Mkongomani huyo, alionekana kutekeleza vyema majukumu yake huku akizunguka eneo lote la kiungo kwa kushirikiana na Mganda, Khalid Aucho mbele yao alicheza Stephane Aziz Ki.
Kasi na uwezo wa kunyang'anya mipira alionao Nzengeli ilikuwa ni faida kwa Yanga ambayo ilionekana kumtegemea zaidi Aziz KI katika utengenezaji wa nafasi  katika eneo la mwisho la ushambuliaji.


VIKOSI
JKT Tanzania;  Yakubu Suleiman, George Wawa, David Bryson, Edson Katanga, Issa Haidary, Said Ndemla, Chiza Kichuya, Hassan Maulid, Matheo Athony, Hassan Kapalata na Sixtus Sabilo.

Yanga; Djigui Diarra, Kouassi Attohoula Yao, Nickson Kibabage,Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca', Khalid Aucho, Maxi Nzangeli, Augustine Okrah, Joseph Guede,Stephane Aziz KI na Kennedy Musonda.