NJE YA UWANJA: Chanzo kupotea kwa Mabondia wa uzito wa juu

Miaka ya 1990 hadi 2000, mashabiki wa ndondi walilazimika kukesha wakisubiri kushuhudia nani ni mbabe wa dunia, miamba yenye mbavu nene ikionyeshana uwezo wa makonde.

Kama si Mike ‘Iron’ Tyson basi ni Evander Holyfield, Michael Spinks, Lennox Lewis, Frans Botha, Andrew Golota, Vitali Klitschko na miamba mingine iliyotamba kwenye uzani wa juu wakati huo.

Baadaye walikuja kina Wladimir Klitschko, Davis Haye, Calvin Brock na sasa dunia inasubiri kwa hamu pambano la miamba, Tyson Fury wa Uingereza na Oleksandr Usyk wa Ukraine.

Wakati dabi hiyo ikisubiriwa kwa hamu duniani kama litatiki, nchini kwa miaka zaidi ya 10, mashabiki wameukosa ule uhondo wa ndondi za mabondia wenye mbavu nene, hakuna tena zile dabi zilizowahi kusimamisha shughuli na kufunga baadhi ya mitaa jijini Dar es Salaam.

Miaka ya 2000 hadi mwishoni mwa 2012, ngumi za uzani wa juu nchini, ziliteka soko, mashabiki waligawanyika wakisubiri kuona ni nani mbabe wa uzani wa juu, wengine walisafiri kutoka maeneo mbalimbali nchini kushuhudia uhondo wa mapambano ya uzani wa juu ambayo ni moja ya alama za ngumi duniani.

Japo Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa anasema nchi imekosa mabondia wa uzani wa juu kwa kuwa waliopo hawana roho ya Simba kumudu kupigania uzani huo, baadhi ya mabondia wa uzani wa juu wanaamini chanzo cha kuadimika ni maslahi.

“Labda tufanye hamasa tukatafute watu warefu wenye miili kule Mwanza au Musoma ili waingie kwenye ngumi, kwa sasa ni kweli hamasa ya uzani wa juu haipo, wanaokuja hivi sasa hawana roho ya simba, wana roho ya sisimizi,” anasema Palasa.

Anasema kupigania uzani wa juu si mchezo, inahitaji uwe na uwezo kweli wa kupigania uzani wa juu, jambo ambalo kwa miaka ya karibuni watu hao kwenye ngumi nchini hawapo.

Promota maarufu aliyewahi kuandaa mapambano kadha wa kadha ya dabi za ‘heavy weight’ nchini, Shomari Kimbau anasema kumuhumia bondia wa uzani wa juu si jambo jepesi.

“Hapa nchini wamekosa watu wa kuwapromoti na kuwasimamia, mabondia wa uzani wa juu huduma zao ni za kipekee, Tanzania kwa sasa hatuna mapromota wa kuwasimamia.

“Kupigania uzani wa juu sio jambo dogo, ile ni kama kifo, ukisikia ngumi nzito ni pale, uzani wa juu una jumlisha mambo mengi, tofauti na hizi nyingine ndogo ndogo, hivyo hata huduma zao ni za tofauti, hapa nchini hawapati watu wa kuwasimamia,” anasema.


Duniani mambo yako hivi

Hivi sasa dunia inalisubiri pambano la Fury na Usyk, bondia namba moja na namba mbili, atakayemshinda mwingine siku watakapokutana ndiye atakuwa kinara wa ulimwengu wa uzani huo.

Mabondia hao kwa sasa wamegawana mataji ya ubingwa na kwa nyakati tofauti wamewahi kupishana kileleni, ingawa kwa mujibu wa Mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec), Fury ambaye kambi yake imeingia kwenye vita ya maneno Usyk ndiye kinara.

Katika 10 bora ya dunia, Anthony Joshua (Muingereza) ni namba tatu, bondia huyo aliwahi kuwa kiara kabla ya kuchapwa na Andy Ruiz (Mmarekani) na kuondolewa kwenye ‘ufalme’ wa uzani wa juu na Ruiz kukaa kwa muda kileleleni kabla ya kuporomoshwa na sasa Fury bondia ambaye hajawahi kuonja ladha ya kipigo anatawala.

Fury, Usyk, Joshua na Ruiz wote wana nyota tano, wakifuatiwa na Joe Joyce (UK) na Deontay Wilder (USA) wenye nyota nne na nusu, wakati Dillian Whyte, Luis Ortiz, Daniel Dubois na Joseph Parker wakihitimisha 10 bora ya dunia.

Bondia aliyewahi kuja nchini, Kubrat Pulev ni wa 12, akiwa nyuma ya Derek Chisora aliyekamata nafasi ya 11 wakati, Muafrika,

Martin Bakole wa DR Congo anayeishi Scotland akiwa wa 14 na Mnigeria, Afe Ajagba anayeishi Marekani akiwa wa 17 duniani.


Bongo iko hivi

Awadh Tamim ni bondia pekee wa uzani wa juu aliyepo kwenye ‘Top 10’ ya Afrika ya uzani wa juu akikamata nafasi ya sita nyuma ya vinara Bakole na Ajgba, Kevin Lerena (Afrika Kusini), Raphael Akpejiori (Mnigeria anayeishi Marekani) na Keaton Gomes wa Afrika Kusini wakiingia kwenye tano bora.

Kidunia, Tamim anayeishi Stockholm ni wa 149 kati ya 1372, rekodi ambayo ameitengeneza akiwa nje ya nchi na karibuni alitwaa ubingwa wa Sweden na mwaka jana alitwaa mkanda wa Europa, amewahi kuwa bingwa wa taifa wa uzani wa juu na Afrika Mashariki na kati kabla ya kwenda kuishi Sweden miaka kadhaa iliyopita.

Katika rekodi, Tanzania ina mabondia 12 wa uzani wa juu, ingawa kati yao ni Tamim pekee ana rekodi bora, aliyecheza mapambano 21 na kushinda 15, bondia namba mbili nchini, Jafari Shayo amecheza pambano moja na kupigwa, anayefuatia, Hamisi Palasungulu amecheza mara saba na kushinda mara nne.

Wengine wa uzani wa juu nchini ni Victor Mashaka, Lugano Mwaikambo, Ramadhani Ally, William Chenge, Kalolo Kahumwa, Said Mndolwa, Saidi Mohamed na Baraka Mwaipaja.

Mabondia maarufu wa uzani wa juu, Alphonce Mchumiatumbo na Shaban Hamadi Jongo, sasa wako nafasi ya pili na ya nane nchini kwenye uzani wa cruiser.

Mchumiatumbo aliyewahi kuwa namba moja kwenye uzani wa juu, ameshusha uzani na sasa niwa nane na Jongo ni wa pili nyuma ya Karim Mandonga bondia namba moja nchini kwenye uzani huo.

Ukiachana na ubingwa wa juzi wa PST, ambao ni mkanda wa kawaida, Mandonga hana ubingwa mwingine au rekodi ambayo inamuweka kwenye renki bora kidunia kama ilivyo kwa ilivyo kwa wengine 12 walio chini yake kwenye uzani wa cruiser ambao bondia wake anaweza kupigana na yule wa uzani wa juu.

“Changamoto ya mabondia wa uzani wa juu nchini, si wale wenye sifa hasa za kupigania uzani wa juu,” anasema Tamim na kufafanua kwamba.

“Nchini wengi wameingia kwenye ngumi na kuwa ma-heavy weight kwa kuwa tu ni wanene, wameshawishiwa kupigania uzani wa juu, lakini hawana sifa hizo, ingawa wapo wenye sifa na hawataki kucheza ngumi, hiyo ndiyo changamoto.

“Nakumbuka wakati niko Tanzania, mapambano ya uzani wa juu yalikuwa na mvuto na yalikuwa ndiyo mapambano makuu, lakini sasa, linaweza kupigwa pambano, lisiwepo hata moja la uzani wa juu,” anasema.

Anasema ukiachana na udhamini kuwa mgumu na promosheni, inaonyesha mabondia waliopo wa uzani wa juu wamekata tamaa, wengine ni waoga na baadhi yao hawajiamini akisisitiza, uzani wa juu una vitu vingi kama sio mvumilivu utaishia njiani.

“Mapambano ya uzani wa juu yana hadhi fulani, lakini kwa Tanzania ni kama mvuto umepotea, huenda waliopo hawafanyi vizuri, lakini bado kuna fursa ya kurejesha ile hadhi yake kama ilivyokuwa zamani, binafsi niko tayari kurudi nikipata ushirikiano kuirudisha hadhi ya mapambano ya uzani wa juu,” anasema.

Hata hivyo, Mchumiatumbo amekuwa tofauti kidogo na Tamim akisisitiza kwamba, maslahi kiduchu ndiyo ytamewakimbiza mabondia wengi kupigania uzani wa juu.

“Kuna mabondia walijaribu, wamecheza mapambano kama mawili bure wakaacha, maslahi ndiyo yanwakimbiza wengi, mfano promota anataka kukulipa laki tatu kwa pambano, ukiangalia mazoezi yako hata hiyo pesa haitoshi, unaona bora ufanye kazi nyingine,” anasema.