Tyson Fury alivyomaliza ubishi wa Wilder

Sunday October 10 2021
tyson pic
By Matereka Jalilu

ILIKUWA ni kisasi au kumaliza ubishi kati ya mabondia wawili wa uzito wa juu Duniani (Heavyweight), Deontay Wilder na Tyson Fury.

Baada ya mapambano mawili yaliyoanza na droo mwaka 2018, kabla ya Tyson Fury kumtandika Deontay Wilder kwenye pambano la pili kwenye raundi ya saba, pambano la tatu limemaliza ubishi kati yao.

Wilder ndiye alitakiwa kulipiza kisasi na alianza kuonesha ari kubwa ya kufanya hilo kwenye raundi za mwanzoni, ikiwemo kumdondosha mpinzani wake (Fury) mara mbili.

Tyson Fury hakutaka kumpa nafasi Wilder kummaliza baada ya kurudisha mashambulizi akifanikiwa kumuangusha mara mbili kabla ya kumuangusha mara ya tatu na ya mwisho kwenye raundi ya 11 iliyomaliza pambano hilo.

Fury alifanikiwa kumaliza pambano kwa Knockout (KO) kwenye raundi hiyo ya 11 baada ya kumtandika makonde mfululizo hususani kwenye sikio la kushoto la Wilder, ikiwa ni marudio ya alichokifanya kwenye pambano la pili mwaka jana kwa kumpiga katika eneo lile lile.

Ushindi huo ukimaanisha kwamba Tyson Fury amemaliza ubishi wa Deontay Wilder, akitetea mkanda wake wa WBC dhidi yake ambaye alitakiwa kupigana naye mwishoni mwa mwaka jana ikashindikana kwa kutokua sawa, baadaye mwaka huu akatibua pambano la Fury na Anthony Joshua kwa maamuzi ya mahakama.

Advertisement

Fury sasa amefikisha mapambano 31 aliyoshinda bila kupoteza na sare moja dhidi ya Wilder, ambapo atasubiri mapambano mawili mbele yake akianza na kutetea mkanda wa WBC dhidi ya Dillian Whyte.

Whyte ana pambano dhidi ya Otto Wallin Oktoba 30, ambapo akishinda anaweza kumpa changamoto Tyson Fury, wakati ambao pia Fury atakuwa anasubiri hatma ya pambano la marudiano baina ya Oleksandr Usyk na Anthony Joshua, kujua bondia yupi atakutana naye kwenye pambano lingine la kuwania mikanda ya uzito wa juu.

Advertisement