NYUMA YA PAZIA: Unamkumbuka James Rodriguez? Yuko hoi

UNAPOJIKUMBUSHA kwamba Lionel Messi ana miaka 35. Unapojikumbusha kwamba Thiago Silva ana miaka 37. Unapojikumbusha kwamba Luka Modric ana miaka 37. Unapojikumbusha kwamba Cristiano Ronaldo ana miaka 38. Kuna jambo usijisahau kujikumbusha.

Jikumbushe kwamba kuna mchezaji anaitwa James Rodriguez ana miaka 31 tu. Hao wote waliotajwa juu yake ni kaka zake ambao wamemzidi umri kuanzia miaka mitano. Umemkumbuka James Rodriguez? Yule staa wa kimataifa wa Colombia.
Tunavyozungumza, achilia mbali Ronaldo ambaye amekwenda ligi nyepesi Uarabuni, hao wengine wote wanacheza timu kubwa na katika kiwango cha juu. Lakini juzi tu, James alikuwa amechaniwa mkataba wake na klabu ya Olympiacos ya Ugiriki.

Ameruhusiwa kuondoka klabuni hapo kama mchezaji huru.
Ungeweza kudhani katika umri wa miaka 31, James angekuwa mchezaji huru ambaye hatamaniwi na klabu yoyote kubwa barani Ulaya? Ni jambo la kushangaza. Huu ndio umri wa kuwa mwendo mdundo, huku ukicheza kiwango cha juu. Lakini kwa James inashangaza kwamba jua kwake limezama.

Nyakati zimekwenda wapi kwake? Haijapita hata miaka kumi alikuwa mmoja kati ya wachezaji bora duniani. Haijapita hata miaka kumi alikuwa mmoja kati ya wachezaji ghali duniani. Real Madrid walilipa kiasi cha Euro 80 Milioni kuinasa saini yake kutoka Monaco ya Ufaransa.

Madrid walilazimika kulipa kiasi hicho baada ya James kuonyesha ubora wake katika Kombe la Dunia. Ndani ya mechi tano tu za Kombe la Dunia mwaka 2014 pale Brazil James alikuwa amefunga mabao sita na kupiga pasi mbili za mabao, huku akiipeleka Colombia katika robo fainali ya michuano hiyo. Nani asingelipa pesa hiyo? Wababe Madrid walipeleka hizo Euro katika akaunti ya Monaco na hakuna ambaye angewalaumu.

Msimu wake wa kwanza ulikuwa mzuri. Alichaguliwa katika kikosi cha msimu cha La Liga. Msimu wake wa pili ndipo nuksi ya maisha yake ya soka ilipoanzia. Alikutana na Rafa Benitez ambaye hakumpenda James, pia yeye (James) mwenyewe akakutana na majeraha ya muda mrefu.

Baada ya hapo akaenda zake Bayern Munich kwa mkopo ambako alipelekwa na Carlo Ancelotti aliyekuwa kocha wake katika msimu wake wa kwanza Real Madrid. Hata hivyo mambo yalikwenda kombo. Nadhani hiyo ndio ilikuwa timu yake ya mwisho kubwa kucheza barani Ulaya.

Jaribu kufikiria kwamba baada ya hapo alikwenda zake Everton. Nadhani ni kwamba sababu Ancelotti alikwenda hapo. Nadhani kwake Ancelotti ni kama baba yake. Pale alianza vizuri, lakini hakuweza kurudia yale makali yake aliyotuonyesha katika Fainali za Kombe la Dunia.

Baba yake alipoondoka nadhani naye akalazimika kuondoka zake klabuni. Kilichoshtua ni namna ambavyo mwenyewe alijitafakari na kuona anafaaa kwenda Uarabuni. Akaenda zake Qatar kucheza Al-Rayyan.
Huko pia mambo yalikuwa ovyo na mashabiki walimchoka mapema wakaanza kumzomea. Kiwango chake kilikuwa duni na alikuwa na majeraha ya mara kwa mara kiasi kwamba mashabiki walikuwa wanamzoea na kuona anakula pesa yao bure. Kule pia walichana mkataba.

Baada ya hapo, Septemba mwaka jana James alikwenda zake Ugiriki kucheza Olympiacos. Amedumu miezi saba tu na juzi Alhamisi wamekubaliana kuachana. Kwa sasa hana timu. Jaribu kumfikiria James yule wa wakati ule kwamba eti angefika miaka 31 akiwa kama nyanya iliyooza sokoni.
Sijui atakwenda wapi, lakini nadhani inaweza kuwa atarudi Uarabuni au ataenda zake Marekani. Siku hizi pia huwa wanakimbilia hata Brazil kama ambavyo Luis Suarez amefanya. Kwa chochote kilichomtokea James nasubiri kwa hamu kusoma kitabu chake.

Wakati mwingine wachezaji wa aina ya James huwa wanakabiliwa na vitu vingi nyuma ya pazia. Mwishowe wanapomaliza maisha yao ya soka huwa wanafichua kile kilichokuwa kinaendelea pindi wanapoandika vitabu vya kuelezea historia ya maisha yao.

Mchezaji mzuri hawezi kumalizika ghafla akiwa kijana. Huwa kuna mambo mengi nyuma yake. Mwingine anaweza kuwa anasumbuliwa na tatizo la ulevi akiwa nyumbani kwake. Wachezaji kama Adriano wa Brazil walikuwa wanasumbuliwa na matatizo ya starehe.

Mwingine anaingia katika kundi la marafiki wabovu ambao anaambatana nao kila anapokwenda kwa ajili ya kufanya starehe kama vile kuvuta unga, kunywa pombe pamoja na kufurahia maisha na Malaya. Wachezaji wa Amerika Kusini huwa wanakumbana na tatizo hili.

Mara nyingi huwa napenda kusoma majuto yao pindi wanapomaliza maisha yao ya soka na kujutia kile ambacho walikifanya wakiwa katika ubora wao. Kuna wachezaji wengi wa kulipwa barani Ulaya na Amerika Kusini huwa hawajitunzi. Pindi wanapopata pesa nyingi wanaendekeza starehe na mengineyo.
Vyovyote ilivyo nadhani tuliuona ubora wa James kwa asilimia 60 tu. Kuna 40 ambayo tunamdai lakini siamini kama anaweza kutupa tena. Ni ngumu kwa baadhi ya wachezaji ambao tuliuona ubora halafu wakapotea halafu wakarudi tena.

Ni kama kile ambacho kilimtokea Philippe Coutinho. Amejaribu kutapatapa, lakini imeshindikana. Ubora wake unaishia pale pale tu tulipomuona na Liverpool. Alipokwenda Barcelona alishuka. Alipokwenda Bayern Munich akashuka. Amerudi England kuchezea Aston Villa ameshuka zaidi.
Siamini eti kama Coutinho anaweza kufanya maajabu na kurudi kama alivyokuwa. Ni kama ambavyo siamini kuwa James anaweza kufanya maajabu na kurudi kama alivyokuwa. Mchezaji wa aina yake alipaswa kama Modric alivyo sasa na bado angekuwa na miaka mitano ya kutamba katika kiwango cha juu.

Vinginevyo ni jambo la huzuni kuona James akiwa hana timu katika umri wa miaka 31 tu. kwanza hatukudhania kwamba katika umri huo angekuwa Ugiriki akichana mkataba wake na timu kama Olympiacos. Kifupi James ni kipaji kingine kilichopotea mapema.