Pamoja Bid na somo la Afcon 2023
Muktasari:
- Kumalizika kwa fainali za Afcon 2023 ambazo zimefanyika mwaka huu, kunafungua milango kwa awamu ijayo ya mashindano hayo ambayo itachezwa mwakani huko Morocco na baada ya hapo, zitaandaliwa kwa pamoja na nchi tatu za Afrika Mashariki, Kenya, Uganda na Tanzania kupitia tenda yao ambayo ilipewa jina la Pamoja Bid.
Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilifikia tamati jana huko Ivory Coast kwa mchezo wa fainali ulizikutanisha Nigeria na Ivory Coast ambazo zilitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ambao ulichezwa Jumamosi baina ya DR Congo na Afrika Kusini.
Kumalizika kwa fainali za Afcon 2023 ambazo zimefanyika mwaka huu, kunafungua milango kwa awamu ijayo ya mashindano hayo ambayo itachezwa mwakani huko Morocco na baada ya hapo, zitaandaliwa kwa pamoja na nchi tatu za Afrika Mashariki, Kenya, Uganda na Tanzania kupitia tenda yao ambayo ilipewa jina la Pamoja Bid.
Itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi tatu kuandaa kwa pamoja fainali za Afcon na jambo la kufurahisha ni kwamba kwa fursa hiyo, tayari timu za taifa za nchi hizo zimejihakikishia kucheza fainali hizo.
Hata hivyo ni miaka mitatu tu imebaki kabla ya kufanyika kwa fainali za Afcon 2027 na kwa kutokana na hilo, mataifa haya matatu yanalazimika kuanza maandalizi mapema ili yaweze kuandaa kikamilifu fainali hizo.
Na sio jambo baya kama yatatumia fainali zilizomalizika jana huko Ivory Coast kujifunza baadhi ya mambo ya msingi ili mambo yasiharibike pindi zitakapofanyika hapa na Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya mambo matatu ya msingi ambayo Kenya, Uganda na Tanzania zinapaswa kuondoka nayo kutoka fainali za mwaka huu.
Maandalizi ya viwanja, miundombinu mapema
Kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja hadi vikafikia hadhi ya kutumika kwa mashindano makubwa kama hayo sio nyepesi na ya muda mfupi hivyo nchi za Kenya, Uganda na Tanzania zinapaswa kujipanga vilivyo kuhakikisha mchakato huo unakamilika kwa wakati ili viwahi muda wa ukaguzi wa CAF.
Kuelekea 2027, nchi hizi tatu kila moja imeweka ahadi ya ujenzi wa viwanja vipya vya soka na kukarabati baadhi ambavyo vipo ili zitimizwe takwa mojawapo la kuandaa fainali hizo, pasipo kusahau pia ujenzi wa viwanja bora na vya hadhi ya juu kwa ajili ya timu kufanyia mazoezi katika kipindi chote cha mashindano.
Ni mwaka wa nne huu sasa, Uganda ambayo ni miongoni mwa nchi zitakazoandaa fainali hizo kupitia Pamoja Bid inahangaika na ujenzi wa Uwanja wa Namboole ambao utakuwa miongoni mwa vitakavyotumika kwa fainali za Afcon 2027 na bado haijaanza ujenzi wa uwanja mpya ambao utaifanya angalau iwe navyo viwili.
Kenya yenyewe bado haijaanza ukarabati wa viwanja vya Moi na Kasarani na pia bado haijaanza ujenzi wa vingine vipya wakati huo Tanzania ikiendelea na ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ujenzi wa viwanja viwili vipya ambavyo serikali imeahidi ukiwa bado haujaanza.
Kumbukumbu zinaonyesha, Ivory Coast ilitumia zaidi ya miaka miwili katika ujenzi na ukarabati wa kila kiwanja hadi vyote sita vikafikia hadhi ya kutumika kwa fainali za Afcon mwaka huu.
Mfano ukarabati wa Uwanja wa Felix Houphet Boigny ulianza Aprili 2020 na ukaja kukamilika Oktoba 2023 wakati ujenzi wa Uwanja wa Olimpiki wa Alassane Ouattara ulianza Desemba 2016 na ukaja kufunguliwa Oktoba 2020.
Ugumu wa mashindano
Ndani ya uwanja, fainali za Afcon mwaka huu zilikuwa za aina yake kutokana na ushindani mkubwa uliooneshwa na asilimia kubwa ya timu shiriki jambo lililopelekea kuwepo na matokeo ya kushangaza katika idadi kubwa ya mechi.
Baadhi ya timu ambazo zilikuwa zikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mashindano hayo zilijikuta zikipata matokeo mabaya ambayo yalizifanya zisitinge hatua za juu za mashindano hayo huku baadhi ambazo hazikupewa nafasi kubwa zikichomoza na kugeuka gumzo.
Ilianzia katika hatua ya makundi ambapo timu nyingi zilizotegemewa zingekuwa wababe wa makundi zilijikuta zikimaliza katika nafasi ya pili, ya tatu na nyingine zikishika mkia.
Guinea Ikweta ilimaliza ikiwa kinara wa kundi A mbele ya Nigeria na Ivory Coast ambazo mojawapo ilipewa nafasi kubwa ya kumaliza ikiongoza kundi, huku kundi B likiongozwa na Cape Verde mbele ya Misri na Ghana wakati huo mshangao mwingine ukiwa katika kundi D ambalo liliongozwa na Angola mbele ya Burkina Faso na Algeria.
Hatua ya 16 bora nayo ilikuja na mshtuko wake baada ya timu mbili zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kutwaa Ubingwa, Morocco na Senegal kuondoshwa zikiungana na Misri.
Hiyo inatoa taswira kuwa fainali za 2027 ambazo Tanzania, Kenya na Uganda zitaandaa kwa pamoja hazitokuwa lelemama na timu zetu za taifa zitapaswa kufanya kazi ya ziada ili zisiishie kuwa wasindikizaji na kupata aibu ya kutolewa mapema huku zikiwa zimeandaa.
Mashirikisho ya soka ya nchi hizi tatu yanapaswa kufanya kazi ya ziada kuzibana idara zao za ufundi kuhakikisha zinatengeneza timu bora na nzuri ambazo zitaweza kuingia kama washindani na sio washiriki.
Kuimarisha ligi na klabu za ndani
Bado Kenya, Uganda na Tanzania hazina nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa katika ligi za ushindani mkubwa na bora barani Ulaya hivyo zinategemea pia wachezaji wanaocheza katika ligi ya ndani katika vikosi vyao vya timu za taifa.
Mashindano ya Afcon yanahusisha timu nyingi ambazo vikosi vyao vinajaza nyota wanaofanya vyema katika klabu zao Ulaya na ili ukabiliane nao ukiwa na kundi kubwa la wachezaji wa ndani, unapaswa kuwa nao wale wenye ubora wa hali ya juu ambao wanaweza kumudu ushindani dhidi ya mastaa hao.
Kuelekea 2027 kiuna ulazima wa nchi zetu tatu kuhakikisha zinaimarisha na kukuza ubora wa ligi zao pamoja na klabu zao ili kundi la wachezaji watakaopata fursa ya kucheza Afcon 2027 liwe na utayari wa kuleta heshima.
Tunaweza kujifunza hili kwa Afrika Kusini ambayo msingi wa mafanikio yake katika fainali za Afcon mwaka huu ni wachezaji wa Mamelodi Sundowns ambao mwishoni mwa mwaka jana waliiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa mashindano ya African Football League.
Lakini ubora wa ligi ya Afrika Kusini ambayo ina Mamelodi, umechangia pia kiwango bora cha Namibia ambayo ilikuwa inategemea nyota wengi wanaocheza katika ligi hiyo.
Ndumbaro atamba
Waziri wa utamaduni, sanaa na michezo Tanzania, Damas Ndumbaro alisema kuwa watahakikisha fainali za Afcon 2027 zinakuwa bora na za kihistoria na alifafanua kuwa alienda Ivory Coast ili kujifunza.
“Ni muhimu timu zetu ziwe na ubora wa kutosha na hamasa tutakapokuwa wenyeji 2027 na ndio wajibu wetu kufanikisha hilo.
“Kutokana na kuwa waandalizi ifikapo 2027, madhumuni ya uwepo wangu hapa (Ivory Coast) ni kujifunza kuhusu maandalizi, miundo mbinu, jinsi ya kuandaa tukio lenyewe, mapokezi, hoteli, mashabiki, uwanjani, na mfumo wa tiketi,” alisema Ndumbaro.