Kocha Afrika Kusini alia na kichapo Afcon 2023

Muktasari:

  • Afrika Kusini ilishindwa kwenda fainali ilipochapwa na Nigeria kwa penalti 4-2 kwenye mechi ya nusu fainali.

Abdjan, Ivory Coast. Kocha wa Afrika Kusini, Hugo Broos amesema timu yake ilikuwa inastahili kwenda fainali badala ya Nigeria kwa kuwa ilikuwa na kiwango bora zaidi kwenye mchezo huo wa Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2023).

Afrika Kusini jana ilishindwa kwenda fainali ilipochapwa na Nigeria kwa penalti 4-2 kwenye mechi ya nusu fainali, baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120, kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Bouake.

Broos amesema timu yake ilionyesha kiwango kizuri na ilitakiwa kushinda mchezo huo kwa kuwa ilitawala kila eneo.

“Wakati mwingine matokeo ya soka yanaumiza, kama utaona jinsi ambavyo timu yetu imecheza utaamini kuwa sisi tulikuwa bora, kulikuwa na mkwaju wa penalti katikati, lakini tukapoteza na sasa hatupo kwenye fainali.

 "Ni ngumu kukubaliana na hali hiyo kwa kuwa tulicheza vizuri, nafikiri tulikuwa timu bora kwenye kipindi cha kwanza, tulipata nafasi kadhaa, Nigeria hawakuwa na nafasi yoyote, kipindi cha pili walikuwa na nafasi kidogo, walitumia moja na kupata bao ambalo lilibadilisha kila kitu, kama tungetumia nafasi zetu tulikuwa tunaweza kwenda fainali na siyo Nigeria," alisema.

Afrika Kusini sasa itavaana na DR Congo kwenye mchezo wa mshindi wa tatu Jumamosi, huku Nigeria ikivaana na Ivory Coast kwenye fainali, Jumapili.