Prime
Parker aanza na mapya Simba
Muktasari:
- Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa huo mara nne ikiwa ni timu ya pili kwa mafanikio kwenye michuano hiyo inayoshirikisha timu 10 kwa mwaka huu.
Kocha mpya wa Simba Steven Parker jana aliondoka na jeshi lake kwenda visiwani Zanzibar huku akibadilisha mambo mengi kwenye kikosi hicho.
Simba itacheza mchezo wake wa kwanza wa michuano ya Kombe la Mapinduzi kesho dhidi ya Muembe Makumbi kwenye Uwanja wa Amaan kikiwa ni kipimo cha kwanza cha kocha mpya wa timu hiyo.
Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa huo mara nne ikiwa ni timu ya pili kwa mafanikio kwenye michuano hiyo inayoshirikisha timu 10 kwa mwaka huu.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Simba haijampa presha kubwa kocha huyo kwenye michuano ya Mapinduzi kutokana na kutofanya maandalizi ya kutosha na kuwa na wachezaji wachache kutokana na wengine kuwa na timu za taifa, lakini ikiwa imemtaka ahakikishe timu yake inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kuchukua ubingwa wa CRDB Federation ambao unashikiliwa na Yanga.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya Simba, kimesema kuwa kocha huyo anatakiwa kuhakikisha anatimiza malengo hayo ili kuendana na matarajio ya klabu hiyo, lakini mwenyewe ameshaanza na mabadiliko kwenye utaratibu wa kikosi hicho huku akitaka wachezaji wakae kambini kwa muda mrefu, lakini pia sasa mazoezi ni mara mbili hadi tatu kwa siku.
"Huyu kocha ndiyo anaanza kutengeneza benchi lake, lakini anaonekana kuwa na misimamo mikali na moja ya jambo ambalo ameshawaambia wachezaji wake ni kwamba anafanya kazi na mchezaji mwenye nidhamu, anayesikiliza na kujituma mazoezini.
"Amesema kwa sasa ambapo timu ipo Mapinduzi na hata ikirudi Dar itakaa muda mwingi kambini tofauti na ilivyokuwa kipindi cha Dimitar Patev ambaye timu ilikuwa inaingia kambini siku mbili kabla ya mchezo, lakini pia mazoezi yatakuwa mara mbili kwa siku hadi tatu.
"Amesema kutakuwa na mazoezi ya asubuhi, jioni na wakati mwingine wachezaji wataanzia kwenye mazoezi ya Gym asubuhi au jioni ndiyo waende kwenye mazoezi ya uwanjani," kilisema chanzo hicho.
"Kuna vitu vingi kabadilisha, kuna hata suala la chakula kuna jinsi anavyotaka wachezaji wakiwa kambini wale, naona kutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye kipindi chake toifauti na watangulizi wake," kilimalizia chanzo hicho.
Parker raia wa Afrika Kusini, kabla hajajiunga na Simba alikuwa kocha mkuu wa Stellenbosch inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini ambayo ilikutaka na Simba kwenye hatua ya nusu fainali katika michuano ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita na kutupwa nje ambapo Simba ilikwenda fainali na kuchapwa jumla ya mabao 3-1 na Berkane.
Simba inatafuta ubingwa wake wa kwanza baada ya kupita miaka minne mfululizo kombe hilo likichukuliwa na Yanga, lakini pia inataka kufika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ikiwa imeshapoteza michezo miwili ya hatua ya makundi na sasa inajiandaa na mchezo dhidi ya Esperance de Tunis ambao umeshikilia hatma yao ya kwenda robo fainali utakaopigwa Januari 23.