Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pasi, umakini kuamua mshindi Stars, Algeria

Nahodha wa Stars, Nadir Haroub “Cannavaro’'

Muktasari:

Stars inaivaa Algeria leo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

Dar es Salaam. Soka la pasi za chini, umakini ndizo mbinu muhimu zitakazoibeba Taifa Stars leo dhidi ya Algeria.

Katika mchezo wa kwanza kati ya miwili ya kuwania kuingia hatua ya makundi kwenye mashindano ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Russia, Stars ina kibarua kigumu.

Stars iliyokuwa mazoezini Afrika Kusini italazimika kutumia mbinu sahihi ili kuwamudu wapinzani wao Algeria, ambao mbali ya uzoefu, uwezo wao mkubwa wa kutumia mipira ya juu, pia wanabebwa na vimo vyao.

Uchunguzi kwenye kikosi cha Algeria umeonyesha kuwa wastani wa urefu wa wachezaji wao ni futi 6 (mita1.83), ikilinganishwa na wapinzani wao, Stars ambao wengi wao ni wafupi, wenye wastani wa futi tano (mita1.52), ukiondoa John Bocco wa Azam, mwenye urefu wa futi 6, inchi 3.

Kwa sababu hiyo, wachezaji wa Stars wanapaswa kumiliki mpira, kupiga pasi fupi, kucheza kwa kasi, lakini kwa pasi zinazowiana na vimo vyao, sanjari na maumbo yao madogo ikilinganisha na wapinzani wao.

Akizungumza na gazeti hili jana, nahodha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa masuala ya soka, Ally Mayay alisema ni lazima Stars icheze aina hiyo ya mpira ili kutowapa mwanya Algeria kuleta madhara.

“Jambo kubwa ni kuhakikisha sisi (Stars) tunamiliki mpira kwa asilimia kubwa kuliko wao (Algeria) kwa sababu wanatuzidi urefu na pia tusifanye makosa ya mara kwa mara kwenye safu yetu ya ulinzi, kwa sababu wale ni wachezaji wenye uzoefu mkubwa kuliko sisi, hivyo ukiwapa nafasi wanaitumia kukuadhibu.

“Pili, ni lazima tuwabane kwenye eneo la kiungo, kwa kucheza mpira wa chini kwa sababu wale wengi maumbo yao ni makubwa, hivyo huwa wanapata taabu kucheza aina hiyo ya mpira na mara nyingi wao hupendelea mipira ya juu.

“Tukitawala kiungo, tutakuwa na nafasi kubwa ya kutengeneza nafasi nyingi za mabao ninazoamini Samatta (Mbwana), Ulimwengu (Thomas) na Maguli (Elius) walioko kwenye ubora wa juu kwa sasa watazitumia vizuri na kufunga mabao yatakayotusaidia.

“Hivyo, kikubwa ambacho benchi la ufundi linatakiwa kufanya ni kupanga wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kutawala mpira kwenye eneo la kiungo ambao tunao wengi,” alisema Mayay.

Aliongeza mchambuzi huyo kuwa ingawa kwenye wa soka ni ngumu, wachezaji kutofanya makosa, jambo pekee ambalo nyota wa Stars hasa mabeki walizingatie ni kutofanya makosa kila wakati.

Alisema makosa ya mara kwa mara ni hatari, linaweza kuigharimu timu kutokana na wapinzani wao kuwa na uwezo mkubwa wa kutumia makosa hayo kufunga.

Nahodha anena

Akizungumzia mchezo huo nahodha wa Stars, Nadir Haroub “Cannavaro’ (pichani) aliliambia gazeti hili kuwa ingawa wanawaheshimu Algeria kama timu bora barani Afrika, watahakikisha wanaibuka na ushindi wa aina yoyote ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya makundi.

“Tunajua tunakutana na timu kubwa na bora si tu Afrika bali duniani kwa ujumla lakini siku zote mchezaji aliyekamilika huwa anatamani kukutana na timu bora ili aweze kuonyesha uwezo wake. Tutahakikisha hatuwapi nafasi ya kucheza na tutapambana tuibuke na ushindi hata wa bao 1-0 ilimradi tu wao wasitufunge au kutoka sare na sisi,” alisema Cannavaro.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika, ikiwamo kuwasili kwa waamuzi kutoka nchini Mali watakaochezesha mechi hiyo ambao waliwasili nchini tangu juzi. Waamuzi huo ni Keita Mahamadou ambaye atakuwa mwamuzi wa kati, akisaidiana na Diarra Bala pamoja na Niare Drissa Kamory. Mwamuzi wa akiba, atakuwa ni Coulibaly Harouna, wakati kamishna wa mchezo atakuwa ni Mukuna Wilfred kutoka Zimbabwe.