Pitso atishwa zigo Uarabuni

Pitso atishwa zigo Uarabuni

ALIYEKUWA kocha mkuu wa klabu ya Al Alhy ya Misri na Memelodi Soundowns ya Afrika ya Kusini, Pitso Mosimane amekianza kibarua chake kipya rasmi kwa kufanya mazoezi  ya kwanza katika klabu mpya ya Saudi Arabia Al-Ahli jana mchana.

Mosimane aliwasili katika jiji la bandari la Jeddah siku ya Jumatatu kuanza kandarasi yake ya miaka miwili kama kocha mkuu katika klabu ya Ahli, ambapo amepewa jukumu la kuirudisha  klabu hiyo kubwa ya Saudi Arabia kwenye Ligi kuu ya nchini humo ijulikanayo kama 'Saudi Arabia pro League'.
Al-Ahli walishuka daraja kwa mara ya kwanza  msimu uliopita na wamemgeukia kocha huyo ambaye wanategemea ataimarisha timu hiyo ambapo viongozi wa timu hiyo walikuwa tayari kumpatia kiasi akitakacho ilikuweza kujiunga nao jambo ambalo lilifanikiwa na kumvuta Pitso nchini humo.

Picha zilizotolewa na klabu hiyo Jumatatu jioni zilionyesha Mosimane hakupoteza muda alipoanza mazoezi yake ya kwanza kwenye Uwanja wa Prince Mohammed bin Abdullah Al Faisal baada ya kutambulishwa kwa wafanyakazi na wachezaji.

Mosimane atakuwa akifanya kazi katika klabu hiyo na wajumbe wa kutumainiwa kama vile mkufunzi wa mazoezi ya viungo Kabelo Rangoaga na wachambuzi wa utendaji Musi Matlaba na Kyle Solomon ambao walifanya kazi naye aliposhinda mataji mfululizo ya Ligi ya Mabingwa ya CAF na CAF Super Cup akiwa na miamba wa Misri Al Ahly.