Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi Tanzania yapanda Ligi Kuu, Prisons yashuka

Muktasari:

  • Polisi Tanzania ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu kwenda Ligi ya Championship katika msimu wa 2022/2023 baada ya kumaliza katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.

Mbeya. Baada ya kudumu kwa misimu 15 mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara, Tanzania Prisons imeaga rasmi ligi hiyo baada ya kukubali kipigo cha jumla cha mabao 4-1 kutoka kwa Polisi Tanzania kwenye mechi za mtoano (Play Off).

Licha ya Prisons kushinda bao 1-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa leo Alhamisi, Julai 16, 2026 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, haikutosha kufuta kipigo cha 4-0 ilichopata kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Ushirika, Moshi, Julai 12.

Matokeo hayo yameifanya Polisi Tanzania kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kukaa nje kwa misimu mitatu tangu iliposhuka daraja mwishoni mwa msimu wa 2022/23.

Kwa historia, Tanzania Prisons imekuwa timu ya tatu kushuka daraja kupitia mfumo wa Play Off, ikizifuata Mbao FC na Mbeya City. Kwa upande mwingine, Polisi Tanzania imeandika historia ya kuwa timu ya tatu kutoka Championship kupanda Ligi Kuu kupitia Play Off, baada ya Ihefu (sasa Singida Black Stars) na Mashujaa FC.

Polisi Tanzania ilimaliza msimu uliopita wa Championship katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 66, kabla ya kuitandika Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1 katika hatua ya awali ya mtoano na kufuzu kucheza dhidi ya Prisons.

Kwa upande wa Prisons, ilimaliza Ligi Kuu nafasi ya 13 ikiwa na pointi 32, na baada ya kushindwa na Mbeya City katika hatua ya kwanza ya Play Off, ikaangukia kucheza na Polisi Tanzania kupigania nafasi ya kubaki Ligi Kuu.

Katika mchezo wa marudiano, kila timu ilicheza kwa tahadhari. Prisons ilihitaji ushindi wa mabao manne ili kubaki Ligi Kuu, huku Polisi Tanzania ikihitaji sare, ushindi au hata kufungwa kwa tofauti isiyozidi mabao matatu ili kupanda daraja.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania Prisons kushuka daraja, baada ya kufanya hivyo msimu wa 2009/10, kabla ya kurejea Ligi Kuu msimu wa 2011/12 na kudumu kwa miaka 13 mfululizo.

Pia ilikuwa mara ya pili kwa Prisons kucheza Play Off dhidi ya timu ya Championship. Mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2021/22, ilipoiondoa JKT Tanzania kwa jumla ya mabao 2-1 na kubaki Ligi Kuu.

Kwa upande wa benchi la ufundi, kocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata ameendelea kuthibitisha ubora wake wa kupandisha timu daraja baada ya kufikisha timu tano alizozipandisha Ligi Kuu. Makata amewahi kufanya hivyo akiwa na Alliance FC, Dodoma Jiji, Pamba Jiji na sasa Polisi Tanzania kwa mara ya pili, rekodi inayomfanya kuwa kinara katika historia hiyo.

Kwa upande wa Prisons, kocha Shedrack Nsajigwa, aliyekabidhiwa timu hiyo akitokea Transit Camp, ameonja uchungu wa kushuka daraja katika msimu wake wa kwanza kuinoa timu ya Ligi Kuu.

Baada ya filimbi ya mwisho, Uwanja wa Sokoine uligeuka kuwa wa shangwe kwa wachezaji na mashabiki wa Polisi Tanzania waliokuwa wakisherehekea kurejea Ligi Kuu, huku upande wa Tanzania Prisons ukitawaliwa na simanzi baada ya kupoteza nafasi yao kwenye ligi ya juu.