Prisons yaikomalia Yanga, Simba yafufua matumaini

SULUHU ya bila kufungana kati ya Yanga dhidi ya Tanzania Prisons imewafanya mashabiki na viongozi wa timu hiyo watoke kichwa chini katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa upande mwingine matokeo hayo ni kama yanairejesha mchezoni Simba ambao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 46 na Yanga wakishika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 57 na kufanya kuwe na tofauti ya pointi 11 tu.

Kipindi cha kwanza kwenye mchezo wa Yanga dhidi ya Tanzania Prisons, timu hizo zimetoshana nguvu baada ya kitokuwa aliyeona lango la mwenzake.

Yanga ilionekana kuhitaji bao la kuongoza lakini mipango yao ilikuwa inakwama kwenye umaliziaji.

Penalti ya kipindi cha kwanza aliyokosa Fiston Mayele inaweza ikawa ni pigo kwa Yanga ambalo hawatolisahau wakiwa kwenye mbio za ubingwa.

Kipindi cha pili Prisons ilifanya mabadiliko ya kuingia Michael Ismail na Adil Buha huku wakitoka Samson Mbangula na Vedastus Mwihambi.

Yanga nao dakika  56 ilifanya mabadiliko ya kumtoa Jesus Moloko na kuingia Denis Nkane na Diara Djigui alitoka ambaye alionekana kuingia na nafasi yake aliingia Abuutwalib Mshery.

Prisons ilionekan kucheza nyuma zaidi na hata walipokuwa wanapiga mipira mbele ilikuwa inapotea kutokana  na kutokuwa na wachezaji wao wengi golini.

Dakika 64 Yanga ilifanya mabadiliko mengine ya kumtoa Kibwana Shomari na kuingia Farid Mussa.

Dakika 66 Yanga ilikosa bao baada ya Feisal Salum kuingia na mpira mpaka ndani ya boksi na kuoiga shuti lililopanguliwa  na kipa Hussein Abel na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Yanga ilifanya mabadiliko mengine dakika 70 akitoka Salum Abubakari ‘Sure Boy’ na kuingia Heritier Makambo kwenda kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.

Mabadiliko ya Sure Boy yalionekana kupingwa na mashabiki wengi waliokuwa uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kuzomea lakini kocha Nasreddine Nabi alimpongeza mchezaji huyo.

Yanga ilikuwa inaoyesha kuhitaji bao huku upande wa Prisons wao hata sare kwao ilikuwa sawa.

Dakika 76 kiungo mkabaji wa Prisons, Jumanne Elfadhil na madaktari wa timu hiyo walionyeshewa kadi za njano na kufanya wawe wa kwanza kuonyeshewa kadi hizo.

Yanga dakika 81 ilifanya mashambulizi mfululizo lakini kuweka wavuni ilikuwa changamoto kutokana na umakini wa mabeki wa Prisons ulioongozwa na Nurdin Chona.

Saido Ntibazonkiza wa Yanga alionyeshewa kadi ya njano dakika 86 baada ya kumfanyia madhambi Michael Ismail n wakati huo huo Prisons ilifanya mabadiliko ya kumtoa Jeremiah Juma na kuingia Mohamed Mkopi.

Yanga ilikosa bao la wazi dakika 89 baada ya Fiston Mayele kumtoka beki wa Prisons, Nurdin Chona na kukimbia kwa spidi ndani ya boksi na kupiga pasi mkunjo ya chinichini (V) lakini mshambuliaji mwenzake, Heritier Makambo aliukosa mpira huo ambao kama angeugusa ungeenda wavuni.