Rais Mwinyi atia neno Kombe la Muungano

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Miaka 60 ya Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Kitabu cha Safari za Picha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 60 kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024.

Muktasari:

  • Baada ya kutangazwa kurejeshwa kwa Kombe la Muungano Rais wa Zanzibar Dk Huseein Mwinyi amewakaribisha wananchi kwenda kushuhudia mashindano hayo.

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema ni wazo zuri aliloamua Rais Samia Suluhu Hassan kurudisha kombe la Muungano kwani watakuwa wamethamini Muungano kwa kurudisha kombe hilo hivyo amewakaribisha wananchi kwenda Zanzibar kushuhudia mashindano hayo.

"Tukushukuru kwenye sekta ya michezo Rais Samia umeona sasa turudishe kombe la Muungano,"amesema Dk Mwinyi.

Hayo ameyasema leo Aprili 24,2024 jijini Dodoma kwenye uzinduzi wa vitabu viwili vya miaka 60 ya historia ya ofisi ya makamu wa Rais na Kitabu cha Safari ya picha ya Muungano.

Taarifa za kurejea tena kwa kombe la Muungano nchini ilitolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiwa imepita miaka 20 tangu kusimama kwa mashindano hayo mafupi yataanza Aprili 23, mwaka huu kwa kujumuisha timu za Zanzibar na Tanzania Bara.

Mashindano hayo yatafanyika Kisiwani Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complez ikiwa ni kuelekea kilele cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, mashindano hayo msimu huu yatashirikisha timu nne zilizothibitisha kushiriki Zikiwemo mbili za Bara ambazo ni Simba na Azam FC wakati kutoka Zanzibar wamo mabingwa wa Kisiwani humo KMKM na KVZ.

Mapema Yanga inaelezwa iliomba kutojumuishwa kwenye mashindano hayo kwa kile ilichoeleza kubanwa na ratiba.