Rais Samia aingilia kati sakata la Fei Toto, Yanga

Muktasari:

  • Fei Toto aliingia kwenye mgogoro wa kimkataba na waajiri hao wa zamani  Yanga na kuamua kuvunja mkataba huku akijiondoa kikosini.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wa Yanga kumaliza sakata la kiungo, Feisal Salum maarufu kama Fei Toto.

 Yanga na Feisal, wameingia katika mgogoro wa miezi kadhaa sasa, tangu mchezaji huyo alipoamua kuvunja mkataba na klabu hiyo.

Mara kadhaa, uongozi wa klabu ya Yanga umeibuka ukimtaka afuate utaratibu kwa mujibu wa sheria za kuvunja mkataba.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni na Yanga, iliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam leo, Juni 5, 2023 Rais Samia aliutaka uongozi wa klabu hiyo kumalizana na mchezaji huyo.

“Sasa kabla ya kufunga viongozi nina ombi kwenu, mmeomba kwangu nami naomba kwenu, sifurahii kusikia mnakuwa na mizozo na wachezaji, sitaki kusema mengi nataka niwaambie tu ishu ya Fei Toto hebu kaimalizeni.

“Kaimalizeni ili tuangalie mbele sasa, haipendezi klabu kubwa kama hii iliyofanya vizuri mnakuwa na kaugomvi na katoto hebu kamalizeni muende vizuri.

“Nitasubiri kupata mrejesho wa hili, siku yoyote mkiwa tayari karibuni nyumbani mje kunipa mrejesho,” Rais Samia Suluhu Hassan.