Refa aipa nguvu Yanga kwa TP Mazembe

Dar es Salaam. Historia ya nuksi ya mwamuzi Lahlou Benbraham (36) kutoka Algeria kwa timu za DR Congo hapana shaka inaiweka Yanga katika hali nzuri ya kujiamini katika mechi ya mwisho ya kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe kwenye Uwanja wa TP Mazembe mjini Lubumbashi leo kuanzia saa 10:00 jioni.

Mwamuzi huyo ambaye amechezesha mechi 32 za mashindano ya klabu Afrika tangu 2016, amekuwa hana upepo mzuri na klabu za nchini humo kwani mara zote alizowahi kuchezesha hakuna hata moja iliyowahi kupata ushindi.

Benbraham katika michezo minne ambayo alikutana na timu za DR Congo katika nyakati tofauti kwenye mashindano ya klabu Afrika, zimepoteza mara mbili na kutoka sare mbili.

Katika mechi ya leo Benbraham atasaidiwa na raia wenzake wa Algeria ambao ni Mokrane Gourari, Akram Zerhouni na Houssam Benyahia.

Ingawa Yanga inaingia katika mechi ikiwa imeshakata tiketi ya kucheza robo fainali, lakini inahitajika kupata ushindi na kuiombea mabaya Monastir ambayo itakuwa nyumbani kucheza na Real Bamako ili iweze kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi, jambo litakaloifanya ikutane na timu iliyomaliza ya pili katika mojawapo kati ya makundi mengine matatu.

Mbali na hilo, ushindi utaifanya Yanga kuandika historia ya kumaliza makundi kwa mara ya kwanza ikiwa inaongoza msimamo wa kundi katika mashindano ya klabu Afrika baada ya kushindwa kufanya hivyo awamu tatu tofauti kwenye hatua hiyo 1998, 2016 na 2018.

Lakini pia hapana shaka itakuwa inataka kufikia rekodi ya Simba ya kuwa timu ya Tanzania iliyokusanya idadi kubwa ya pointi katika makundi ya mashindano ya klabu ambapo watani wao walivuna pointi 13 katika hatua hiyo Ligi ya Mabingwa Afrika 2020/2021.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema wanahitaji kupata ushindi ili wamalize wakiwa vinara wa kundi. “Tunatakiwa kuingia hatua inayofuata tukiwa tunaongoza kundi,” alisema Nabi.