Rombo Marathoni kuhamasisha utalii

Muktasari:

  • Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema katika sikukuu za mwisho wa mwaka kipindi ambacho wilaya hiyo inapokea wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali watatumia nafasi hiyo kuanzisha Rombo Marathoni ili kuhamasisha utalii katika wilaya hiyo.

  

Rombo. Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema katika sikukuu za mwisho wa mwaka kipindi ambacho wilaya hiyo inapokea wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali watatumia nafasi hiyo kuanzisha Rombo Marathoni ili kuhamasisha utalii katika wilaya hiyo.

Profesa Mkenda ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia ameyasema hayo wakati wa mchuano wa mashindano ya fainali ya 'Mkenda cup"yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika  Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.

"Sisi Warombo wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka (christmas) tunakuja kupumzika kula ndafu sasa wakati wa kula ndafu Warombo wote popote walipo duniani tunaanzisha Rombo Marathoni kwa ajili ya wale ambao watakuwa hapa.

"Tutaanza mapema maandalizi ya Rombo Marathoni ambayo tutakimbia kuanzia barabara ya Lower road kwa lengo la kuchangamsha na kuhamasisha utalii katika wilaya ya yetu ya Rombo,"amesema Profesa Mkenda

Mkenda amesema katika kuhitimisha mashindano hayo ya mbio za Rombo Marathoni kutakuwa na tamasha la wasanii wa Rombo waliopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kutambua michango yao katika Taifa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga amesema amesema Ubunifu wa Profesa Mkenda katika wilaya hiyo  umekuwa ukiwaunganisha Worombo wote na kuwa kitu kimoja katika mambo mbalimbali yenye tija.