Ronaldo aipeleka Ureno fainali akifunga bao
Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40 alifunga bao hilo katika dakika ya 68, akiunganisha pasi ya Nuno Mendes.
Munich, Ujerumani. Mshambuliaji wa Ureno Cristiano Ronaldo ameonyesha bado ana uchu wa ushindi baada ya kufunga bao la ushindi lililoipeleka timu yake katika hatua ya fainali ya UEFA Nations League kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ujerumani.
Mchezo huo uliopigwa katika jiji la Munich ulianza kwa kasi ambapo dakika ya 48, kinda wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz, aliiweka Ujerumani mbele kwa bao la kichwa akiunganisha krosi ya Joshua Kimmich.
Ureno haikukatishwa tamaa kwani katika dakika ya 63, Francisco Conceição, ambaye alikuwa ameingia kutokea benchi alitumia dakika tano tu kufunga bao la kusawazisha baada ya kuwatoka mabeki wa Ujerumani na kufunga kwa kisigino mpira uliompita kipa wa Ujerumani, Marc-Andre ter Stegen.
Dakika tano baadaye, nahodha wao Cristiano Ronaldo, aliifungia Ureno bao la ushindi akimalizia krosi iliyopigwa na Nuno Mendes. Bao hilo linakuwa la 137 kwa Ronaldo katika timu yake ya taifa akiendeleza rekodi ya kufumania nyavu mara nyingi akiwa na timu hiyo.
Baada ya ushindi huo, timu ya taifa ya Ureno imetinga katika hatua ya fainali ya michuano hiyo ya mataifa Ulaya ambapo itamsubili mshindi wa nusu fainali itakayopigwa leo kati ya Hispania dhidi ya Ufaransa.
Hii ni mara ya pili Ureno inatinga katika fainali kwani mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2019 walipotinga fainali na kuibuka mabingwa baada ya kuifunga Uhoranzi bao moja.
Hizi ni fainali za nne za michuano hiyo tangu kuanzishwa kwakwe ambapo mabingwa wa kwanza walikuwa ni Ureno walipofanya hivyo msimu wa 2018-2019, Ufaransa 2020-2021 pamoja na Hispania 2022-2023.