Hawa hapa wafungaji wa Klabu Bingwa Dunia

Muktasari:
- Katika mashindano ya 2009 na 2011, Messi alishinda tuzo ya mfungaji bora ambapo mara zote hizo Barca ilikuwa bingwa.
Miami, Marekani. Mwezi ujao, macho ya ulimwengu wa soka yatageukia Marekani, ambako kutafanyika mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu, ambapo itakuwa ni muundo mpya utakaohusisha timu 32 bora kutoka mabara yote.
Mashindano hayo yataanza rasmi Juni, 14, 2025 na kuhitimishwa Julai, 13, 2025, yakichezewa katika viwanja 12.
Bingwa mtetezi wa taji hili, Manchester City ya England, waliotwaa ubingwa mwaka 2023 baada ya kuichapa Fluminense ya Brazil kwa mabao 4-0 kwenye fainali iliyopigwa jijini Jeddah, Saudi Arabia ni miongoni mwa timu shiriki kutoka England ikiwa pamoja na Chelsea.
Katika makala hii, tunatazama mastaa ambao wanaongoza hadi sasa kwa kufunga mabao mengi zaidi katika michuano hii kwenye mara kadhaa walizocheza.
SALEM AL-DAWSARI-4, Al-Hilal
Salem Al-Dawsari alikuwa miongoni mwa majina maarufu zaidi katika Ligi Kuu ya Saudi kabla ya mastaa wa Ulaya kuanza kuingia.
Winga huyu ameshiriki Kombe la Dunia la Klabu mara tatu, akifunga mabao manne katika kipindi hicho. Katika mashindano ya 2019/20, alisaidia Al-Hilal kufika hatua ya mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, lakini walipoteza kwa penalti dhidi ya Flamengo.
Aliisaidia tena Al Hilal miaka miwili baadaye kufika hatua ya nusu fainali ambapo walipoteza mbele ya Chelsea kisha wakapoteza kwa Al Ahly katika mchezo wa mshindi wa tatu. Katika michuano yote aliyoshiriki staa huyu alifunga mabao manne.
PEDRO 4, Flamengo
Pedro alitarajiwa kuwa mmoja wa wachezaji bora wa Brazil waliotabiriwa kwamba wangeenda kung’ara Ulaya. Hata hivyo, mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa, licha ya kusajiliwa na Fiorentina.
Ni kama staa huyu iliandikwa atang'aa akiwa Amerika ya Kusini tu kwani alionyesha kiwango bora akiwa na Flamengo, ambako alikuwa na wastani wa kufunga bao kwenye kila mechi mbili.
Hili lilidhihirika katika Kombe la Dunia la Klabu la 2022/23, ambapo akiwa na umri wa miaka 27, alifunga mabao manne katika mechi mbili tu kusaidia timu yake kumaliza nafasi ya tatu.
Mabao yake mawili ya mwisho dhidi ya Al Ahly yaliwafanya watoke nyuma ya matokeo ya 2-1 na kushinda 4-2.
CESAR DELGADO 5, Monterrey
Katika maisha yake ya soka, Cesar Delgado alichezea timu kadhaa, ikiwemo Cruz Azul, Olympique Lyonnais na Atlas. Hata hivyo, alishiriki Kombe la Dunia la Klabu akiwa na Monterrey ya Mexico pekee. Aliiwakilisha timu hiyo kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2012 hadi 2014, akifunga jumla ya mabao matano.
Mchezaji huyu wa kimataifa wa Argentina alikuwa mhimili wa mashambulizi ya timu, akicheza kama winga au kiungo wa kati.
LIONEL MESSI-5, Barcelona
Lionel Messi haihitaji utambulisho. Ni mmoja wa wachezaji bora zaidi wa muda wote. Kutokana na kushinda Ligi ya Mabingwa mara tatu, Messi alishiriki Kombe la Dunia la Klabu mara tatu.
Katika mashindano ya 2009 na 2011, Messi alishinda tuzo ya mfungaji bora ambapo mara zote hizo Barca ilikuwa bingwa.
Mwaka 2015 alimaliza wa pili nyuma ya Luis Suarez katika suala la utupiaji.
LUIS SUAREZ-5, Barcelona
Luis Suarez ni mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea katika kikosi cha Barcelona. Ushirikiano wake na Messi na Neymar ulikuwa wa kuvutia, na uliisaidia Barca kushinda mataji mbalimbali kama Ligi ya Mabingwa dhidi ya Juventus mwaka 2015.
Miezi michache baadaye walishiriki Kombe la Dunia la Klabu na nyota huyo wa zamani wa Liverpool alionyesha makali yake kwa kufunga hat-trick katika nusu fainali dhidi ya Guangzhou F.C., kisha akafunga mabao mawili ya mwisho kwenye fainali dhidi ya River Plate iliyomalizika kwa Barca kushinda 3-0.
Hizo ndizo mechi mbili pekee alizocheza katika mashindano hayo, lakini aliweza kufunga mabao matano na akashinda tuzo ya mfungaji bora kwa mwaka huo.
KARIM BENZEMA-6, Real Madrid/Al Ittihad
Unapozungumza kuhusu washambuliaji bora wa muda wote, jina la Karim Benzema huwezi kuliacha. Alifunga bao muhimu katika fainali ya 2016 dhidi ya Kashima Antlers na kuiwezesha Madrid kushinda michuano ya mwaka huo.
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika fainali nne tofauti za michuano ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka 2023, baada ya kufunga dhidi ya Auckland City akiwa na Al-Ittihad.
GARETH BALE – 6, Real Madrid
Gareth Bale alistaafu mwaka 2023, akiacha historia ya kipekee kutokana na rekodi zake katika michuano mbalimbali.
Bale ambaye alijiunga na Real Madrid mwaka 2013, alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichoshinda mashindano ya Kombe la Dunia kwa klabu mwaka 2014, 2016 na 2017, huku yeye akifunga mabao muhimu na kutoa pasi kadhaa za mabao.
Alifunga bao la pili dhidi ya San Lorenzo kwenye fainali ya 2014, pia katika mashindano ya 2018, alishinda tuzo ya mfungaji bora baada ya kufunga mabao matatu.
CRISTIANO RONALDO – 7, Real Madrid/Manchester United
Cristiano Ronaldo ambaye anatajwa kuwa mchezaji bora wa Ureno wa muda wote. Pia ndio mshambuliaji mwenye mabao mengi zaidi katika michuano hii.
Ronaldo ambaye hadi sasa amezichezea timu tano ikiwemo Sporting Lisbon, Manchester United, Real Madrid, Juventus na sasa Al-Nassr, ameshiriki michuano hii akiwa na timu mbili tu.
Kwanza kabisa ilikuwa na Man United ambapo baada ya kuchukua Ligi ya Mabingwa mwaka 2008, walienda kucheza michuano hii ya Klabu Bingwa Dunia na kufanikiwa kushinda pia wakati huo yeye akifunga bao katika nusu fainali dhidi ya Gamba Osaka.
Akiwa na Madrid alienda kushinda taji hili mara tatu katika misimu miwili alifanikiwa kumaliza kama mfungaji bora wa mashindano.