Ronaldo akosa Kombe Al Nassr ikichapwa na Wajapan
Muktasari:
- Taji pekee ambalo Ronaldo ametwaa akiwa na Al Nassr ni la Ligi ya Mabingwa Uarabuni ambalo timu yake ilitwaa mwaka 2023.
Cristiano Ronaldo ameshindwa kutwaa taji la kwanza kubwa akiwa na Al Nassr baada ya timu yake leo Jumamosi, Mei 16, 2026 kupoteza kwa bao 1-0 mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Asia 2 dhidi ya Gamba Osaka.
Bao la Deniz Hummet katika dakika ya 30, limeipa Gamba Osaka taji la mashindano hayo ambayo yanashika nafasi ya pili kwa thamani barani Asia kwa ngazi ya klabu.
Licha ya Al Nassr kuonekana kupambana kwa muda mrefu kusawazisha bao hilo, Gamba Osaka walikuwa imara kuhakikisha nyavu zao hazitikiswi hadi mchezo ulipomalizika.
Kichapo hicho kimemfanya Ronaldo kushindwa kutwaa taji la pili akiwa na timu na la kwanza kubwa tangu alipojiunga nayo mwaka 2022.
Taji pekee ambalo Ronaldo ametwaa akiwa na Al Nassr ni la Ligi ya Mabingwa Uarabuni ambalo timu yake ilitwaa mwaka 2023.
Matumaini pekee kwa Ronaldo na Al Nassr yamebakia katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambayo wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wake msimu huu.
Al Nassr inahitajika kuibuka na ushindi katika mchezo wa mwisho nyumbani dhidi ya Damac ili ifikishe pointi 86 zitakazoihakikishia taji.
Lakini kama itapoteza ubingwa unaweza kwenda kwa Al Hilal ikiwa itapata ushindi dhidi ya Al Fayha.
Al Hilal ambayo ina pointi 81 hivi sasa huku ikiwa nafasi ya pili, inaweza pia kutwaa ubingwa iwapo itashinda mechi ya mwisho na Al Nassr ikatoka sare na Damac.