Rooney: Everton itatisha msimu huu

Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Everton, Wayne Rooney amesema wachezaji wenzake wapo katika nafasi nzuri ya kuiletea mafanikio timu hiyo katika msimu huu.

Klabu hiyo imeanza safari yake ya kampeni yake kuelekea maandalizi ya msimu mpya kwa kucheza na Gor Mahia ya Kenya  ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu nchini humo msimu ulioisha.

Mchezo huo ambao umevuta hisia za mashabiki na wapenzi wa soka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, inatarajiwa kuchezwa leo Alhamisi jioni saa 11 kwenye Uwanja wa Taifa jijiji Dar es Salaam.

Rooney alisema kurejea kwake kwenye klabu yake ya zamani kutailetea mafanikio klabu hiyo.

Alisema licha ya kuwapo na sura ngeni lakini jambo la furaha kwake na klabu hiyo.

“Klabu imeonyesha matumaini na wachezaji wapo katika kiwango kizuri na tuna vijana wengi. Pia ninaamini klabu ipo kwenye mwelekeo mzuri. Jambo la msingi sasa ni kupata mafanikio. Uhamisho wangu utaimarisha timu yetu,” alisema Rooney wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Waziri wa Habari, Sanaa na Utamaduni, Dk Harrison Mwakyambe.