Roy Keane amponda Erling Haaland

Muktasari:

  • Keane amesema hayo baada ya mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa juzi kati ya Man City iliyokuwa nyumbani ikivaana na Arsenal, mechi iliyomalizika kwa suluhu.

Manchester England. Kiungo na nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane amesema mshambuliaji wa Manchester City Erling Haaland siku za hivi amekuwa akicheza kama mchezaji wa League Two.

Keane amesema hayo baada ya mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa juzi kati ya Man City iliyokuwa nyumbani ikivaana na Arsenal, mechi iliyomalizika kwa suluhu.

Kiungo huyo amesema staa huyo wa Norway amekuwa na kiwango cha chini sana kwa kipindi cha hivi karibuni ndiyo maana haishangazi kuona amegusa mpira mara chache zaidi ya wachezaji wengi kwenye mchezo huo.

Mabeki wa Arsenal, Gabriel na William  Saliba walionyesha uwezo mkubwa wa kumzuia mshambuliaji huyo anayeongoza kwa kufunga mabao kwenye Ligi Kuu England.

"Kwa ujumla mchezaji huyo alicheza vibaya, siyo leo tu nafikiri ni tatizo la muda mrefu kidogo, naona anatakiwa kujirekebisha tena sana, anacheza kama mchezaji wa ligi ndogo, yaani League Two na hana madhara.

"Amekuwa ni mchezaji mahiri, anajua kufunga, lakini siyo kwenye kila mchezo, tazama Arsenal wametumia mbinu kidogo tu anaonekana kukasirika, anaonekana wa kawaida kabisa uwanjani, hii siyo levo ya mchezaji mkubwa," alisema Keane.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 23, aligusa mpira mara 23 tu kwenye mechi hiyo, hakupiga shuti langoni, hakutoa pasi yoyote yenye madhara huku akiwa ameshindwa kufanya vizuri kwenye michezo yote ambayo wamekutana na Arsenal.

Mchezo wa juzi ulikuwa wa kwanza kwa timu hiyo ya Pep Guardiola kushindwa kufunga bao nyumbani tangu Oktoba 2021, lakini ukiwa wa kwanza kupiga shuti moja tu lilolenga lango baada ya majaribio 12.

Matokeo haya yameifanya City ibaki nafasi ya tatu, pointi moja nyuma ya Arsenal na mbili nyuma ya vinara Liverpool iliyopata ushindi wa 2-1 dhidi ya Brighton, juzi.