Ruto kama Samia, aahidi noti za kumwaga Harambee Stars
Muktasari:
Timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars' inashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kwa mara ya kwanza tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2009.
Siku 10 baada ya kutangazwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutoa ahadi ya Sh 1 bilioni kwa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ikiwa itatwaa ubingwa wa mashindano ya CHAN 2024, Rais wa Kenya, William Ruto naye ameahidi donge nono kwa timu yake 'Harambee Stars' ikiwa itafankiwa kubakisha taji hilo nyumbani.
Rais huyo ameahidi kitita cha Shilingi 600 milioni za Kenya (Sh12 bilioni za Tanzania) ikiwa Harambee Stars itafanikiwa kuchukua ubingwa kwa kupata ushindi katika mechi zote za mashindano hayo.
Kiasi hicho cha fedha kimegawanya kama bonasi ya ushindi kuanzia katika hatua ya makundi, robo fainali, nusu fainali na fainali.
Ruto ametoa ahadi hiyo leo Jumamosi, Agosti 2, 2025 wakati alipotembelea kambi ya Harambee Stars iliyopo katika Hoteli ya Pullman jijini Nairobi, kuzungumza na wachezaji wa timu hiyo.
"Ninafahamu kwamba bonasi ya kufanya vizuri ambayo ilipangwa na Katibu wa Michezo ingewapatia Sh200 milioni (Sh4 bilioni), Nimeamua kuizidisha mara tatu. Haiwezi kuwa vizuri zaidi ya hivi. Kila mmoja anatakiwa kufanya kilicho bora zaidi," amesema Ruto.
Rais Ruto ametangaza mgawanyo wa Sh12 bilioni hizo utakavyokuwa katika kipindi chote cha mashindano ambacho Harambee Stars itakuwepo.
Kwa mujibu wa Rais Ruto, kila mechi ambayo Harambee Stars itapata ushindi kwenye mashindano hayo, kila mchezaji atapata Sh1 milioni ya Kenya sawa na Sh19 milioni.
Na mechi ambayo itamalizika kwa matokeo ya sare kila mchezaji wa Harambee Stars atapata Sh500,000 ya Kenya.
Fedha hizo zitakuwa zikiongezeka kadri ambavyo Harambee Stars itakuwa inasonga mbele kwenye fainali hizi ambazo zinafanyika katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.
Rais Ruto pia amewataka Wakenya kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao ya taifa na kwa sasa waweke tofauti zao kando ili kuiwezesha timu yao kufanya vizuri.
Julai 24, 2025, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Palamagamba Kabudi alisema Rais Samia ameahidi kutoa Sh1 bilioni ikiwa Taifa Stars itatwaa ubingwa wa fainali za CHAN 2024.
"Katika kuchagiza hamasa kwa timu yetu ya Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya donge nono la fedha za Kitanzania shilingi bilioni moja kwa vijana wetu wa Taifa Stars iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano haya ya CHAN 2024," alinukuliwa Waziri Kabudi.