Saido akiwasha huko Simba aiwinda Prisons

MASHABIKI wa Simba juzi walikatwa stimu baada ya kushindwa kumuona uwanjani kiungo fundi wa mpira aliyesajiliwa kutoka Geita Gold, Saido Ntibazonkiza aliyeishia kukaa jukwaani wakati timu hiyo ikiichapa KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hata hivyo, taarifa ziwafikie mashabiki hao kwamba, kiungo mshambuliaji huyo aliyekwamishwa na vibali kwenye mchezo huo, mambo yake yapo freshi, huku akiendelea kukiwasha kama kawaida mazoezini na kuwapa mzuka wachezaji wa timu hiyo sambamba na benchi la ufundi la Simba.

Kama mipango itaenda ilivyo, basi mwamba huyo huenda akashuka uwanjani leo kupambana na Tanzania Prisons katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mabosi wa Simba walishindwa kupata mapema vibali vya nyota huyo wa zamani wa Yanga anayeichezea pia timu ya taifa ya Burundi, kuanzia vile vya kufanyia kazi na walikuwa wakihaha kuvisaka ili kuvipata mapema wakisaidiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mwanaspoti limedokezwa kwa muda wa siku tatu tangu juzi, uongozi wa Simba ulikuwa ukifuatilia vibali hivyo na mambo yalikuwa freshi ili jamaa aanze na maafande hao ambao jana waliwekewa mzigo mezani wa Sh 30 Milioni kama wataibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

Kama mambo hayatakwenda tofauti kwa mamlaka hizo zenye kutoa vibali, ishu itakamilika muda wowote kabla ya mchezo dhidi ya Prisons na atakuwa kati ya wachezaji 20, ambao wataiwakilisha Simba kwenye mechi ya mwisho kabla ya kikosi hicho kwenda Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi.

Uongozi wa Simba umemalizana tayari na uongozi wa Geita Gold katika kiasi cha pesa ilichokuwa inahitaji kwa ajili kumuachia Saido aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

“Saido tayari amefanya mazoezi nasi Mo Arena Bunju, anaonekana kuwa yupo fiti sana, nafikiri atatusaidia kwenye michezo ya ligi na ile ya kimataifa,” kilisema chanzo kutoka mazoezini Simba.