Saliboko, Nonga wamtishia nyau Kagere ufungaji bora

Muktasari:

Kagere anaongoza msimamo wa wafungaji bora akiwa amefunga mabao nane wakati Saliboko na Nonga wote wamefikisha mabao sita kila mmoja.

Dar es Salaam. Vita ya kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara imezidi kupamba moto baada ya washambuliaji wawili wa Lipuli, Daruweshi Saliboko na Paul Nonga kufikisha mabao sita wakiwa nyuma kwa mabao mawili kwa kinara Meddie Kagere wa Simba.

Kagere anaongoza msimamo wa wafungaji bora akiwa amefunga mabao nane wakati Saliboko na Nonga wote wamefikisha mabao sita kila mmoja.

Mabao matatu aliyofunga Saliboko na mawili ya Nonga katika mchezo wa jana Jumatano kati ya Lipuli dhidi ya Singida United yametosha kuwapaisha wachezaji hao hadi katika nafasi ya pili katika msimamo wa wafungaji na kumkaribia Kagere.

Kagere mfungaji bora wa msimu uliopita kwa mabao 23, leo Alhamisi jioni anayo nafasi nyingine ya kuongeza magoli yake iwapo ataifungia Simba dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wachezaji wengine wanaofuatia katika chati ya wafungaji ni Athuman Miraj wa Simba, Peter Mapunda (Mbeya City), Yusuf Mhilu (Kagera Sugar) na Gerald Mathias Mdamu wa Mwadui wenye mabao manne kila mmoja.

Hat trick ya pili.

Mabao matatu aliyofunga Saliboko katika mchezo wa jana kati ya Lipuli na Singida United yamemfanya mshambuliaji huyo kuwa mchezaji wa pili kufunga hat trick tangu msimu huu wa Ligi Kuu Bara uanze.

Saliboko aliiongoza timu yake kuifanyia mauaji Singida kwa kuichapa mabao 5-1 huku mabao mengine mawili yakifungwa na Paul Nonga.

Mchezaji wa kwanza kufunga Hat trick ni Ditram Nchimbi wa Polisi Tanzania aliyefunga katika mchezo dhidi ya Yanga uliofanyika Oktoba 3 na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.