Schmeichel: Man United wamemsajili kipa asiye sahihi
Muktasari:
- United itaikaribisha Chelsea katika Uwanja wa Old Trafford wikiendi hii, na kocha Ruben Amorim ana kibarua cha kuamua iwapo atamwamini Lammens au kuendelea na Altay Bayindir.
Manchester, England. Aliyekuwa golikipa gwiji wa Manchester United, Peter Schmeichel, ameonyesha kutoridhishwa na usajili wa kipa mpya wa klabu hiyo, Senne Lammens, akisema hakuwa hata amewahi kumsikia kabla ya dili hilo la Pauni Milioni 21.
United ilimchukua Lammens kutoka Royal Antwerp ya Ubelgiji, huku kipa wa zamani Andre Onana akipelekwa kwa mkopo Trabzonspor. Hata hivyo, Schmeichel anaamini uongozi wa timu hiyo umekosa mwelekeo.
“United walipaswa kumsajili Emiliano Martinez wa Aston Villa. Hata Donnarumma tulikuwa na nafasi ya kumsajili awali, na wote ni makipa wenye uzoefu mkubwa,” amesema Schmeichel kupitia mahojiano na SunSport.
Schmeichel aliongeza kuwa, ingawa takwimu za Lammens zinaonekana nzuri, bado hajathibitishwa katika kiwango cha juu cha ushindani.
“Kwa uaminifu, sikuwahi kumsikia Lammens hadi tetesi zilipoibuka. Takwimu pekee haziwezi kukuonyesha namna unavyoshughulika baada ya kufanya kosa, au jinsi ya kuhimili presha ya Manchester United,” amesema kipa huyo wa zamani wa United.
Lammens, mwenye umri wa miaka 23, anachukuliwa kama nyota anayekuja, lakini Schmeichel ameonya kuwa ni hatari kwa United kumtegemea kipa kijana kwenye nafasi nyeti.
Kwa upande mwingine, Martinez alihusishwa sana na uhamisho kwenda Old Trafford na inadaiwa alitamani kujiunga, lakini dili halikukamilika.
Man United itaikaribisha Chelsea katika Uwanja wa Old Trafford wikiendi hii, na kocha Ruben Amorim ana kibarua cha kuamua iwapo atamwamini Lammens au kuendelea na Altay Bayindir.
Peter Schmeichel alizaliwa1963 nchini Denmark na anachukuliwa kama moja ya makipa bora kabisa katika historia ya soka. United walimsajili kutoka Brøndby IF mwaka 1991 kwa kiasi cha pauni laki nane pekee dili ambalo baadaye Sir Alex Ferguson aliita “usajili bora zaidi wa karne”.
Akiwa golini, Schmeichel alijulikana kwa urefu wake, ujasiri na staili yake ya kipekee ya kuokoa mashuti kwa kutumia mikono na miguu. Alikuwa pia nahodha na mara nyingi ndiye aliyepiga kelele zaidi uwanjani kuwasimamia mabeki wake.
Kilele cha mafanikio yake kilikuwa mwaka 1999, alipokuwa nahodha kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa huko Camp Nou, Barcelona, baada ya Roy Keane na Eric Cantona kukosekana. United walipindua matokeo dhidi ya Bayern na kushinda mataji makuu matatu (Treble) ya kihistoria (Premier League, FA Cup na Ligi ya Mabingwa Ulaya).
Schmeichel aliondoka United baada ya msimu huo na kuelekea Sporting Lisbon, lakini jina lake lilibaki kwenye vitabu vya rekodi kama mmoja wa wachezaji muhimu zaidi kwenye enzi ya dhahabu ya Sir Alex Ferguson.