Serengeti Boys yaanza vibaya Afcon U17 ikilala mabao 5-4

Muktasari:

  •  Awali katika dakika 45 kipindi cha kanza Serengeti Boys walijikuta wakichezea kichapo cha mabao 3 -1.  

TIMU ya Taifa Tanzania chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' imepoteza mchezo wake wa kwanza baada ya kukubali kufungwa mabao 5-4 dhidi ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi Fainali za Vijana Afcon 2019 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Awali katika dakika 45 kipindi cha kanza Serengeti Boys walijikuta wakichezea kichapo cha mabao 3 -1.

Katika mchezo huo Nigeria ndio walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 19 kupitia kwa Olatomi Olaniyani baada ya piga nikupige kutokea langoni mwa Serengeti.

Hata hivyo Serengeti Boys hawakuonyesha kukata tamaa baada ya kufungwa goli hilo walianza mpira kwa haraka na kupiga mpira mrefu ulioenda kwa Kelvin John ambaye alipiga pasi ya mwisho kwa Edmund John na kuifungia goli Serengeti ndani ya dakika 20.

Baada ya goli hilo Serengeti Boys waliinuka na dakika 26 Kelvin John 'Mbappe' alitoka na mpira kwa spidi akiwa katikati na kuwatoka mabeki wa Nigeria na kupiga shuti hata hivyo lilipanguliwa na kutoka nje.

Nigeria nao walizidi kufunguka na kuonyesha kuhitaji magoli na dakika 28 mbinu yao ilijibu baada ya kupata goli kupitia kwa Wisdom Ubani. Vijana wa Serengeti Boys hasa katika upande wa mabeki walionekana kukatika hali hoyo ilizidi kuwapa nafasi vijana wa Nigeria kucheza. Dakika 36 Nigeria walipata goli la tatu dakika 36 baada ya mabeki wa Serengeti kuzani mshambuliaji wa Nigeria, Akinkunmi Amoo kuchomoka na mpira haraka na kuweka mpira wavuni.

KIUNGO TATIZO

Katika mchezo huu kikosi cha serengeti Boys kilionekana kuwa na shida katika eneo la kiungo baada ya mara kwa mara kukatika.

Hali hiyo iliwafanya viungo wa Nigeria kutawala zaidi na kucheza kwa namna ambavyo wanataka. Kocha Oscar Mirambo wa Serengeti alifanya mabadiliko katika eneo la kiungo dakika 17 kwa kumtoa Misungwi Chananja na kumuingiza Edson Mshirakandi.

Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuonyesha kuzaa matunda katika eneo hilo la kiungo mpaka dakika 55.

Hata hivyo hadi dakika ya 72 Serengeti Boys walikuwa wamesawazisha mabao na kuwa 4-4 lakini vijana wenzao wa Nigeria walipambana na kujipatia bao la tano. Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa matokeo ya  Tanzania kufungwa mabao 5-4.