Serikali yatoa neno ishu ya Fei Toto

SAKATA la Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yanga limemwibua Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya michezo nchini, Ally Mayay na amewashauri wachezaji wa Kitanzania kuwa na mameneja ambao watawasimamia mambo yao ikiwemo suala la mikataba.

Hatua hiyo imekuja baada ya Feisal na Yanga kuwa na mgogoro wa kimkataba uli0malizwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kudai mchezaji huyo ni mwajiriwa wa Yanga.

Kiungo huyo alivunja mkataba wake na Wanajangwani hao ili kuwa huru kujiunga na timu nyingine huku akiweka kitita cha Sh112 milioni kwenye akaunti ya Yanga.

Akizungumzia ishu ya Fei, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema Serikali ni wazazi na wanaomba jambo hilo limalizwe ili mchezaji huyo aweze kucheza.

“Wote ni wadau wa michezo tunataka mafanikio kwa hiyo tunaomba masuala haya yamalizwe, pande zote mbili ziwe zimekubaliana kwa sababu sisi Serikali ni wazazi tunataka mafaniko ya wote.

“Kikubwa ni kuangalia kasoro kama hizi zisitokee tena ili kuhakikisha pande zote mbili zimefanikiwa, wakifanikiwa wao ndio Serikali imefanikiwa,” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Mayay ambaye amewahi kuzichezea timu za CDA, Yanga na timu za Taifa ‘Taifa Stars’ alisema:

“Moja ya mapungufu mengi ambayo tunayo ni kutokuwa na mameneja ambao wanawasimamia na kila kitu kinakuwa wazi lazima awe mwenye uwezo au mwanasheria kuwa na meneja kwa sasa hakukwepeki,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mayai amewataka wachezaji wa Kitanzania kutodanganya umri kwa masilahi ya Taifa.

“Sasa hivi michezo ni ajira lazima kuwe na matumizi sahihi ya umri na umri ni kitu sahihi, unacheza kipindi kidogo sana ukifika miaka 32 unaitwa ni mkongwe.

“Kwa manufaa ya kwao na Taifa ni kitu cha muhimu sana, wenzetu wanapewa sana semina, lazima ufikirie mbali hata kama huna hata shilingi,” alisema.